JINA LA KITABU: DHAMBI YA MOYO
MWANDISHI: ALI SULEIMAN ALI(Al-Salmy)
Watsapp: 0777749669
Mawasiliano :0658745759
SURA YA KWANZA
Yalikua ni majira ya asubuhi inayojivutavuta
kutoka alfajiri, jua lenye rangi nyekundu ndio hiloo linachomoza kutoka
mawinguni likiwa linasambaza mwanga mwembaamba katika dunia.
Ni katika kijiji cha Wasahawa vikionekana
vibanda vingi vilivyosheheni pamoja ambapo wamiliki wa vibanda hivyo walikuwa
wanavitumia kama ndio sehemu ya makaazi yao. Vilikuwa ni vibanda vilivyo
sanifiwa kwa umbo la nyumba vilivyozibwa kwa kutumia udongo mwekundu pamoja na
nyasi zilizosimama kutokana na jua la siku nyingi.
Sauti
ya huruma ilisikika kutoka kibandani ikisema
“Mbaraka!!Mbaraka!!... mwanangu…naomba uamke
sasa ili uwahi shambani mapema na pia uwahi kurudi mapema maana leo ni jumamosi
ndio siku pekee ambayo unapata muda wa kutusaidia kazi za hapa nyumbani, kwani
baba yako ndio kwanza amelala nahisi atakua hayuko vizuri maana sio kawaida
yake hii…..”
Ilikua
ni sauti ya mama wa Mbaraka akiwa amesimama nje ya mlango wa chumba cha Mbaraka,
mkononi akiwa ameshika sufuria lililokua na maji machafu.
Mbaraka ni kijana mwenye umri
usiozidi miaka ishirini na miwili, alikuwa na urefu usiopungua futi 5 na nchi 4,
alikuwa ni mweusi wa maji ya kunde mwenye asili ya kibantu. Ni kijana alieumbika
kisura na hata kiumbo pia, alijazia nyusi na nywele nyeusi zenye mng’aro kiasi
ambacho alikuwa na mvuto wa kila aina kwa waschana wengi.
Aliitika kauli ya mamaake na kuenuka kutoka
katika kitanda cha kamba kisichohimili vishindo vya aina yoyote. Baada ya hapo
aliingia chumbani kwa baba yake bila kugonga hodi na kumkuta Mzee akiwa haelewi
chochote kinachoendelea katika ulimwengu huu, hii ni kutokana na machofu ya
siku ya jana shambani yaliyompatia usingizi mzito. Alimuamsha polepole na
kumuaga kwamba anaenda shambani. Mzee Mkata alimuitikia vyema mtoto wake bila
kinyongo na ndipo aliendeleza usingizi wake uliokuwa umebakia nae Mbaraka
aliianza safari ya kuelekea shambani.
Ardhi
ilikuwa kavu sana kutokana na jua kali pamoja na ukosefu wa mvua kwa muda mrefu,
hali ambayo ilimsababisha kuchoka mapema na kupoteza maji mengi kwa njia ya
jasho.
Ilifika
saa tatu, ndipo alikamilisha kazi aliyojipangia kwa siku ile. Hakua na muda wa
kupoteza alisogea bondeni zaidi ambako kulikuwa na mto mdogo wenye maji mazuri
na baridi yasiyokauka katika chemchem hiyo. Alikoga hapo na kusafisha kila
kilchochafuka wakati wa kazi.
Mbaraka
Alirudi nyumbani na kumkuta mama yake amekwisha muandalia chai mzuri kutokana
na uwezo wao. Ulikua ni muhogo wa kuchemsha na mchuzi wadagaa . Walijumuika
pamoja na kujipatia chai iliyoweza kuwasaidia kwa muda wa masaa machache. Hii
ni kutokana na umasikini uliokuwa unawaandama kila kukicha.
Jumapili iliwadia, asubuhi na mapema kama
ilivyo kawaida ya kijana Mbaraka huitumia vyema siku hiyo kwa ajili ya
kujisomea sana ili kutaka kuukabili vyema mtihani wa kidato cha sita unaomnyemelea
kwa siku za mbeleni.
Alikuwa ni kijana aliyethamini sana maendeleo yake yashule na kuzidisha juhudi kila siku
zilivyoendelea mbele ili kuhakikisha anafaulu vyema na kuendelea na masomo ya
chuo kikuu,kwani alikuwa na ndoto za kutaka kuikomboa familia yake ambayo kwa ujumla imekabiliwa na umasikini
mkubwa.
Kila siku alibuni mbinu mpya ambazo zingeweza
kumwongezea hamu na kasi ya kusoma. Kwa kiasi kikubwa alifanikiwa juu ya hilo.
Takriban
walimu wote walimpenda na kumthamini sana kutokana na nidhamu pamoja na
jitihada zake kwenye masomo, jambo ambalo lingeweza kumletea mabadiliko na
maendeleo makubwa siku za mbeleni.
Ilibaki
miezi miwili tu Mbaraka kukabiliana na mtihani mkuu wa taifa wa kidato cha 6, hivyo
juhudi za kusoma zilikuwa nyingi sana.
SURA YA PILI
Katika
kipindi chote hicho maumivu makali yaliukabili moyo wa Bahati aliekuwa binti mrembo
katika kijijicha hicho cha wasahawa, alikuwa ni binti mwenye mvuto wa aina yake
ambao uliwafanya wanaume wengi waliokosa heshima na hata wenye heshima
kutokushindwa lakusema pindi wanapopishana nae. Alikuwa ni msichana mwenye
rangi ya maji yakunde yaliyozidiwa nguvu ya weupe usioisha. Hakuwa msemaji, bali
heshima na upole ndio ulitawala katika himaya yake.
Alikua ni mwenye huruma sana hususani pale
anapoona matatizo ya aina yoyote yanamkabili mwenzake, hakujali rangi, kabila
wala dini, bali kilichokua mbele yake ni ukarimu.
Alipenda
sana kuwa ni binti mwenye elimu ila hakuwa ni mwenye kulifanikisha hilo kutokana
na mila na desturi za familia yake ambao waliona ni uovu mkubwa kwa binti wa
kike kupewa elimu ya shule, hivyo alikuwa akiishi na wazazi kama mtoto wa
nyumbani na kukabiliwa na majukumu pamoja kazi zisizoisha.Huo ulikuwa ni wajibu
wake muhimu kutokana na mtazamo potofu wa wazee wake.
Takribani
wakaazi wote wa kijiji hapo walimuelewa Bahati kwa sifa zake mzuri alizokuwanazo,tatizo
kubwa lililomkabili ilikua ni sifa ya aibu ambayo ilikua inampa maumivu makali ya moyo juu ya kijana Mbaraka.Aliamini
kwamba maisha yake yangekuwa na furaha pale siku atakapokuwa anaishi pamoja na
Mbaraka.
Kwa muda
mrefu uzuri na mvuto wake ulianza kufifia kama mwangaza wa jua la magharibi
kuelekea usiku. Mawazo ya kimapenzi yalimtawala kila wakati katika kichwa chake
juu ya kijana Mbaraka ambae hakujua kilichokua kinaendelea katika moyo wa binti
Bahati.
Kila alichokuwa anakifanya katika maisha yake aliona
kama hakiendi sawa. Hupoteza muda wake mwingi kukaa chumbani na kumuwaza Mbaraka
pasi na mafanikio. Maradhi hayakuwa yakimuacha mkono, kwani mawazo juu ya Mbaraka
yalizidi kila kitu juu ya maisha yake.Alikua akipoteza muda mwingi sana kukaa akitafakari
ni wapi angeanzia ili Mbaraka aweze kumwelewa na akithamini kile kilichomo
ndani ya moyo wake.
Siku zilizidi kusonga,na Bahati alionekana
kuwa tofauti sana mbele ya macho ya mama yake.
Mama Bahati alianza kujawa hofu juu ya afya ya
mototo wake. Baada ya chakula cha mchana ambacho Bahati alishindwa hata kutimiza
tonge tano katika idadi yake, ndipo alipoamua kwenda kujitupa kitandani kusudi
kumwandama Mbaraka katika mawazo yake.
Mama
Bahati kwa siku nyingi hakutaka kulivumilia hilo.Nae aliamua kumfuata chumbani
kutaka kujua nini haswa kimemsibu mtoto wake ambae ndio hazina yake ya pekee.
Alipofika chumbani alimkuta akiwa amejifunika
shuka mithili ya mgonjwa alieandamwa na baridi kwa muda mrefu.
Alimuuliza mwanawe “Bahati mwanangu ulishakufa
na kubakia mzoga tu……”
Bahati
alishangaa kusikia maneno hayo kutoka kwa mama yake “kwanini mama mbona sijakuelewa?”,
Aliuliza Bahati.
“Kwasababu mwanangu Bahati alikuwa hayupo
hivi.Sidhani kama ni wewe,nahisi kuna kitu unanificha kwa muda mrefu sasa au
unaujauzito unanitafutia balaa hapa kijijini…?”
Bahati alijibu kwa upole na heshima kwa mama
yake “hapana mama…ila uchovu tu ndio unanisumbua...si unajua ardhi ya shamba
imekauka sana, hivyo nakua nachoka sana na si vyenginevyo”.
Mama
Bahati hakutaka kujua mengi kwasababu
alimuamini sana mwanawe kwani hakuwa anenda kinyume na maadili yao, hivyo
alimpa moyo mwanawe kwa kumwambia ipo
siku yataisha hayo,yote yalikua ni mapito tu. Aliyaongea hayo na kumuacha mwanawe
akiendelea kubaki chumbani na yeye alienda kuendelea na kazi yake ya kusuka na ukili
na kumata tumbaku chini ya mti mdogo uliokuwa unaficha mwangaza mkali wa jua
nje ya kibanda chao.
Kiukweli Bahati alikuwa anaumizwa sana na
hisia za mapenzi juu ya Mbaraka na tayari yalikuwa maradhi makubwa kwake.
Mtihani wa kidato cha sita kwa Mbaraka ulikaribia
na matumaini ya mafanikio sasa yalianza kupotea.Baada ya taarifa kutoka
serekalini kwamba” KWA MUJIBU WA SHERIA ZA KISEREKALI, HATORUHUSIWA MWANAFUNZI
YEYOTE KUFANYA MTIHANI WA KIDATO CHA SITA KAMA HATOLIPAFEDHA TASLIMU SHILING
40,000”
Kiasi
hicho cha fedha hakikuwahi kumilikiwa hata siku moja katika familia ya mzee Mkata
tangu kuanza kuyafahamu na kuyaelewa maisha yake. Baada ya taarifa hizo kuskika
ndipo Mbaraka alianza kupoteza matumaini na ndoto zake alizokuwa amezipanga.
Mawazo
ya Bahati yalitawala katika mapenzi ya Mbaraka wakati mawazo ya Mbaraka yalitawala
katika kutafuta msaada wa fedha ili kukamilisha ndoto zake. Kwa vile kijana Mbaraka alikua maarufu sana
katika kijijihapo kutokana na heshima zake, basi taarifa za kutokukubalika
kufanya mtihani wake wa taifa kutokana na ukosefu wa fedha iliskika kwa kila
mmoja kijijini hapo.
“Baba,
unadhani ndoto zangu zitaweza kutimia namna hii?, nahisi kuiaga dunia mapema
sana babaangu,umaskini wetu ndio sababu yakutaka kusambaratisha matumaini
yangu.” Mbaraka alisema hayo kumwambia baba yake wakiwa wameketi nje ya nyumba
yao wakitafakari ni wapi wangeapata msaada.
“Usijali
mwanangu hakika Mungu anasikia kilio chako wala usikate tama,kwa vile siku bado
zipo basi na matumaini bado yapo” alimliwaza mwanawe katika hali hiyo ya
msongamano wa mawazo.
Mawazo
yaliwatala sana vichwani mwao.Hakuna aliyejua aanzie wapi wala amlizie wapi
katika kulikamilisha hilo.
Mzee Mkata hakukata tamaa katika kukamilisha
ndoto za mwanawe kipenzi,Siku ya pili ilipowadia alijaribu kupita kwa majirani
ili aweze kuazimwa fedha hizo kusudi alikamilishe hili,kwani alijuwa umuhiu wa
elimu kwa mtoto wake,na pia alizijali sana juhudi za mtoto wake.
“ Ama kweli mtaji wa maskini ni nguvu zake
mwenyewe” kauli hiyo ilikua ikimpitia kichwani mwake kila wakati baada yakuona
matumaini yanazidi kufifia,hakutaka kukata tamaa,alizidi kujaribu kwa hata
asiowajua vyema,lakini kila alivyokuwa akijaribu juhudi hizo hakuweza kupata
matumaini kutokana na umasikini ambao ulitawala kijijini hapo.Kwa kiasi kikubwa
hakuna aliyeweza kumpatia fedha hizo hata theluthi yake.
Aliamua
kurudi nyumbani kwani jua lilikua ni kali sana.
“mwanangu Mbaraka,sistahiki lawama kwako wala
kwa Mungu juu ya hili,nimejitahidi sana,nimedhalilika sana hata kwa
nisiowaelewa vyema,lakini nimeambulia patupu”Aliyasema hayo mzee Mkata akiwa
amekaa juu ya mkeka pamoja na mke wake,huku Mbaraka akiyasikiliza vyema maneno
ya baba yake.
Machozi
yaliyokuwa yamejificha kwa kasi yalianza kutiririka machoni mwa mzee Mkata. Mbaraka
na mama yake waliwajibika kufuta machozi hayo wakati hakuna aliewajibika kufuta
machozi ya Mbaraka na mama yake.
Huzuni
ilitawala katika nyumba yao kwani jitihada za wote ziligonga ukuta.
Kwa vile mapenzi ya kweli
hayajifichi hata kwa siri ya moyo wa mmoja wapo,lingeweza kutimia hili baada ya
Bahati kusikia taarifa hii.Bahati alimpenda sana Mbaraka kiasi ambacho alikuwa
tayari kumpatia fedha hizo kwa siri,hii ni baada yakusikia kutoka kwa watu
tofauti kwamba Mbaraka hatoweza kufanya mtihani wake kutokana na ukosefu wa
fedha.
Kwa kipindi kikubwa Bahati
alikuwa na fedha hizo ambapo hakuna yoyote aliekuwa anatambua juu ya uwepo wa
fedha hizo ambazo aliachiwa marehemu babu yake ambaye alimuusia kuwa asiweze
kuthubutu kuzitoa fedha hizo kwa mtu yoyote ila kwa tatizo kubwa ambalo litaweza
kujitokeza katika familia tu.Bahati aliyakumbuka sana maneno hayo ya marehemu
babu yake yaliyokuwa yakimpitikia kichwani mwake “Bahati mjukuu wangu,nadhani
leo ndio hatma yangu,sidhani kama nitaweza kubakia duniani tena,Mola tayari
ananihitaji,nimekuita chumbani humu peke yako,naitaji kukuachia kiasi cha fedha
na asiweze kutambua mtu yoyote zaidi yako, na pia usijekuthubutu kuzitoa pesa
hizi kwa matumizi isp…po..kuwa kw…a tatizo kubwa ambalo litawez..za kuikumba
familia yako tu, sawa…kwaheri” kauli hiyo ilikuwa inamjia kila wakati kivhwani
mwake.
Lakini mapenzi yaliuzidi
wasia wa marehemu mzee Bakari.Hakua na jinsi ila aliamua kuenuka kitandani na
kusogea karibu na kipembe cha chumba chake huku akichungulia dirishani kwamba
hakuna aliekuwa karibu na chumba chake ambae angeweza kumuona juu ya kile
anachotaka kukifanya.Alichuchumaa chini ya kipembe hicho na kuanza kuchimbua
kwa kisu kilichokuwa kirefu sana.Baada ya sekunde chache alifanikiwa kutoa
kikopo cha kaure ambacho kisingeweza kuharibiwa na mdudu wa aina yoyote. Alinyanyuka
na kusogea kitandani huku akiwa ameshikilia kikopo hicho.Aliketi kitandani na
kutoa mfuko ulikuwemo ndani ya kikopo hicho na kuufungua.Alifanikiwa kutoa
fedha hizo taslimu ambazo zilikua ni shilingi elfu 40.
Baada ya hapo aliwaza ni jinsi gani fedha hizo
zitaweza kumfikia Mbaraka bila ya Mbaraka mwenyewe kuweza kuelewa kwamba pesa
hizo zinatoka kwake.
“Nifanye nini sasa au
nikaziweke chini ya mlango wa nyumba yao?, hapana itakua sio sahihi,naitaji
Mzee Mkata tu peke yake ndio aelewe juu ya fedha hizi na si mwenginewe”. Yalikuwa
ni maneno yaliyokua yakipita kichwani mwa Bahati.
Ghafla wazo jengine lilimjia kwamaba,kwa vile ilikuwa ni asububuhi
ni vyema aweze kwenda shambani kwa Mzee Mkata huenda akaweza kukutana nae,kwani alielewa kawaida ya
mzee Mkata ni kueda shamba kila siku
wakati wa asubuhi.
Kwa vile alielewa kwamba
siku za mitihani zilikuwa zimebaki chache hakuwa na muda wa kupoteza, aliharakia
shambani bila ya hata kumuaga mama yake kwamba anaelekea wapi.
Safari haikuwa fupi na jua
lilikuwa kali sana ila hakuweza kuyahisi maumivu hayo ila ni Mbaraka pekee
ndiyo alikuwemo mawazoni mwake.
Mawazo yake hayakumpoteza kwani ni kweli Mzee Mkata muda huo
alikuwa shambani akiwa analima baada ya kukata tama juu ya pesa ambazo
zingeweza kufanikisha ndoto za mwanawe.
Bahati alikaribia shambani na alisogea
juu ya mlima mdogo akimtazama mzee mkata
akichapuka katika kuwajibika na kazi yake ya ukulima wa viazi.Alisimama hapo
kwa dakika chache akiwaza atamkabilije mzee yule na pia atamwelewaje kwa atanachotaka
kukifanya.
Machozi yalianza kumtoka Bahati
baada ya moyo wake kuzidiwa na mawazo juu ya Mbaraka na shida anazozipata.Kwa
haraka alishika kanga aliyokua amejifunga kiunoni, na kuanza kufuta machozi
yaliyokuwa yakimtoka kwa kasi.Alisogea kwa mzee mkata na kusimama karibu yake
kana kwamba alikua amedhamiria kumuua.
Mzee Mkata hakushangaa sana
hilo, kwani ilikuwa ni kawaida ya mrembo Bahati kupita pale kila asubuhi wakati
anapokwenda kondeni kwao.
“Bahati leo mbona ghafla na
kimya kimya, vipi kwema lakini…?” Mzee Mkata alimuuliza.
“Kwema...Mzee mkata...shikamooo…!!!!”
“Marhabaa...Mzima?, mbona
jana na juzi hukupita kunisalimia..?”
Bahati alianza kupata moyo wakutenda
alichokusudia “hapana mzee nilipita wakati kama huu ila sikukuona nadhani labda
uliwahi kuondoka..”, alijibu Bahati huku akiwa anatabasamu ndani ya moyo wake.
Mzee mkata alisema “ni kweli Bahati siku hizo
nilikuwa nawahi kuondoka mapema kwasababu nilikabiliwa
na kazi kubwa juu ya kijana wangu Mbaraka nilikuwa natafuta wapi ningeweza
kupata fedha kwaajili ya malipo katika mtihani wake wa taifa kwani, huna habari
…?”
Bahati akiwa amejiinamia kwa huzuni “ndio
niliskia na ndicho kilichonileta hapa, niliskia hilo kwa muda mrefu kwamba hatoweza
kufanya mtihani kama hatolipa kiasi cha fedha.Alianza kukitonesha kidonda cha
Mkata kilichokuwa kimeshaanza kupona.
Mzee mkata alianza kujawa na huzuni, kwani
alikwishaanza kuyasahau hayo kwa siku chache. Alimtazama Bahati na kuanza
kumuona kama adui aliekuja kuisumbua himaya yake aliyoimiliki vyema, hakujua
kwamba Bahati alikuja kwa nia njema ambayo ingeweza kumpa furaha daima.
Bila
kuchelewa sana Bahati alitia mkono kifuani kwake na kutoa pesa hizo, machozi
yalianza kumtoka kwa huzuni kuona kwamba mtu anaempenda sana anateseka katika
kutimiza ndoto zake.Hakupenda hata siku moja kuona Mbaraka amefikwa na
matatizo.
Alimuangalia
utadhani hajawahi kumuona katika maisha yake kwani hakuelewa ni nini kunachoendelea
myoni mwa binti Yule.
Wakati
machozi yakimtoka bahati, hakusita kunyoosha mkono wake kwa mzee Mkata, mkono huo
ukiwa na fedha taslim sh/-40000 ambazo Mzee mkata alimaliza juhudi zake zote
katika kutafuta pesa hizo bila mafanikio.Alikua haamini kinachotendeka,alihisi
kama yupo kwenye ndoto.
Wakati
Bahati akimpatia Mzee Mkata fedha hizo alimtamkia “hizi ni pesa taslimu kwaajili ya Mbaraka,naomba
umpatie ili aweze kufanikisha malengo yake ya kielimu,ila nakuomba mzeee...naomba
siri hii iwe ni yangu mimi nawewe tu,nakuomba...nakuomba...nakuomba kama mzee
wangu…fedha hizi zilikua ni hakiba kutoka kwa marehemu babu yangu..” Bahati alimueleza mzee mkata yote bila
kumficha kuhusu wasia wa babu yake juu ya fedha zile.
Mzee Mkata alisimama kama mnara uliojengwa
sikuchache zilizopita. Aliyashayangaa hayo na hakuweza kuongea chochote zaidi
kumuahidi Bahati kwamba hatothubutu kumzungumzia yoyote suala hili.Alimshukuru
sana na aliona kama ni miujiza kutoka kwa mungu.Hakuweza hakuamini
kilichotokea.
Alimshukuru
sana Bahati pasi na kifani, hakujua atamlipa nini binti huyo wala
amshukuru namna gani.Wakati wote huo Bahati hakuweza kuyazuia machozi
yaliyokuwa yakimtoka kwa kasi,na pia
hakuweza tena kustahamili kukaa pale, alikimbia na kuelekea nyumbani kwao.
Haukuchukua muda mrefu, Bahati aliwasili
nyumbani kwa kasi ile ile,alipitiliza moja kwa moja hadi chumbani kwake,wakati
huo mama yake hakuwepo nyumbani ila alienda kuwasalimu majirani zake kama
ilivyo kawaida yake.
Kwa vile Bahati anaelewa sana wasiwasi wa mama
yake pindi amkutapo katika hali hiyo, hakua na budi kujilazimisha kuyazuia
machozi yasiendelee kutoka.
Kadiri siku zilivyokuwa zinaendelea uzuri wa Bahati
ulikua unaendelea kupotea na hali yake kiafya ilizidi kuwa mbaya.Kiukweli mapenzi
yaliusumbua sana moyo wa Bahati.
“Nitaishi
katika hali hii mpaka lini, au kifo changu kinachungwa na mapenzi?, Bahati mimi
,kwanini nisimueleze ukweli Mbaraka, ….atanihukumuje,… hapana, siwezi
kumwambia, nitaichukia jamii kwa aibu kubwa” maneno hayo yalikua yanampitikia
Bahati ndani ya moyo wake akiwa kitandani kwake.
SURA YA TATU
Yalikuwa ni majira ya saa tano
asubuhi Mbaraka akiwa nyumbani kwao akiendelea kujisomea kama kawaida yake kwa kuamini
maneno ya baba na mama yake kwamba asikate tamaa, ipo siku Mungu atasikia kilio
chao.
Wakati
huo mama yake alikuwa yupo jikoni akiendelea na shughuli zake binafsi.Ghafla
alisikia kishindo cha jembe lililoanguka kutoka kutoka katika mabega ya mzee
Mkata.Kwa haraka aliacha kazi zake na kuelekea nje ili aweze kujua nini haswa
kimemsibu kipenzi cha moyo wake.Alimkuta mzee Mkata amesimama na kuelekea jua
na kulipa uso wake huku akiwa ameshika kiuno kwa chake kwa mikono yake yote
miwili. Kikweli mpaka sasa alikuwa hajaamini kile ambacho kimetokea lakini uso
wake ulionesha kutawaliwa na furaha ambayo kwa muda mrefu ilikuwa imempotea.
Bi Mwenda
alimsogelea karibu na kumwangalia usoni hakuna kilichojificha. Aligundua uwepo
wa furaha iliyotawala katika uso wa mume wake.
Bila kumuuliza chochote alichukua jembe na
kuliingiza ndani na ghafla alitoka na kumkaribisha mume wake.
“Haya karibu mume wangu jitayarishe uwahi
kunywa chai mana nahisi una hamu na chai ya leo …”
Mzee Mkata aliitika wito huo wa mke wake na
kujitaarisha kwaajili ya chai,baada ya dakika chache alimuulizia Mbaraka kwani
alikua na hamu ya kumkabidhi yale yote yaliyo moyoni mwake.
“Mbaraka
yupo wapi…? Aliuliza mzee
“Nadhani atakua ndani kujisomea kwani
nilizidi kumuusia kwamba asijaribu kukata tamaa, ipo siku Mungu atasikia kio
chake”, alijibu kwa huzuni bi Mwenda.
“Hahaha!!!,
Tena nileo” aliongezea mzee Mkata huku akiangua kicheko kilichomshangaza mke
wake.
“Mmmm nawewe nawe, mbona umekuja na furaha
leo” aliongea hayo huku akienuka kuenda kumwita mwanawe.
Kwa
bahati mzuri Mbaraka hakuwa mbali.Alikuwepo chumbani akiendelea na majukumu ya
shule.Bi Mwenda aliwajibika kuwakutanisha wote ili waingize tumboni riziki
waliyobarikiwa kutoka kwa Mungu.
Wakati
wakiendelea kujipatia chai mzee Mkata alimuuliza Mbaraka,“Ni siku ngapi ambazo
zimebakia kuingia katika mtihani?”
Mbaraka alijibu kwa huzuni bila kujua nini
alichokusudia baba yake hata akaamua kumuuliza hilo “zimebaki siku tatu tu baba…”
Mzee Mkata hakuona haja ya kusubiria, aliwaeleza
kwamba tayari amefanikiwa kupata fedha hizo zote na kuahidi kwamba kesho
atazifikisha sehemu husika,kwaiyo alimtaka mwanawe aongeze juhudi kwa
kujitayarisha vyema kwa mtihani kusudi aweze kukamilisha ndoto zake alizozipanga.
Bimwenda alijaribu kumuuliza ni nani ambaye
amempatia fedha hizo,lakini mzee Mkata hakuonesha kufurahishwa na swali hilo,bali
alimjibu mke wake kwamba “daima binaadamu wote hawako sawa,wapo wenye navyo,
lakini roho zao ni ngumu kutoa kwa wengine,na wapo wasionavyo lakini mioyo yao
ni milaini kutoa,Mungu amesikia kilio chetu”
Bi
mwenda hakuridhika vyema na jibu hilo kwani alitaka kumjua mtoaji ila kwavile
alimuamini sana mume wake hakutaka kuendelea mbele kwa maswali hayo.
Kiukweli wote walifurahi kwani walijua
mkombozi wao ni elimu ya kijana wao mbaraka juu ya umaskini wao. Hivyo
walipaswa kulijali hilo.
Siku
iliyofuatia mambo yalienda kama yalivyopangwa, Mzee Mkata alifanikiwa kuzifikisha
fedha hizo panapohusika, walimu walifurahi sana waliposkia hilo na pia taarifa
haikusita kuenea kijijini kote.
Siku mbili baadae Mbaraka alikuwa tayari kukabiliana
na mtihani huo, kwani alikuwa amejitaarisha vyema kama majeshi yanayoenda
vitani kukabiliana na magaidi wa dunia.Furaha ilitawala kila kiungo cha Mbaraka
na wazee wake.Wakati huo hali ya Bahati alizidi kudhofu licha ya furaha ndogo
kumuingia moyoni mwake kutokana Mbaraka kufanikiwa kulipa fedha zote.
Masiku yalipita na Mbaraka alifanya mtihani
wake ambao ulifanikisha kumuweka katika idadi ya majina ya wanafunzi waliofaulu
vyema na kujiunga na chuo kikuu cha Dar es alaam.
Mzee Mkata pamoja na mke wake bi Mwenda
walifurahi sana.Kwa mbali walianza kuiona nchi kavu kutoka katika bahari yenye
mkondo mkubwa.
Muda wote yakiwa yanapita hayo kwa furaha Bahati
hakuwa na furaha kwani alijua kifo kinamnyemelea kwasababu afya yake aliyobaki
nayo.
Aliamini
kwamba uwepo wa uhai wake kwa kipindi chote hicho ilikuwa ni kuwepo kwa Mbaraka
kijijini,leo hii Mbaraka anaondoka na hatoweza kumuona tena wala kuskia habari
zake kama alivyozoea.Maneno hayo yalikua ndani ya kichwa chake yakimuumiza
sana.
Bahati
akiwa mwenyewe chumbani alilia sana,ila hakuwa na lakufanya ispokua alienda
kumpatia mzee Mkata zawadi ya pete mzuri aliyokuwa nayo mkononi mwake na
kumtaka mzee Mkata ampatie Mbaraka pindi aondokapo kuelekea Dar es salaam na
amtake ulazima wa kuivaa pete hiyo popote aendapo,hii ingeufanya moyo wake kuwa
na matumaini juu ya mapenzi yake.
“Mzee naomba uchukue pete hii na
umkabidhi Mbaraka pindi atakapoondoka kuelekea huko masomoni ila iwe ni siri
yetu kama lile la mwanzo, mtake aivae na wala asiivue” alisema Bahati kumwambia
mzee baada ya kusalimiana vyema.
Mzee
Mkata nafsi yake ilianza kuchunguliwa na wasaiwasi juu ya siri hizi, lakini
aliyatazama zaidi mafanikio.
Aliyafanya hayo kwa siri yeye na mzee Mkata, hilo
lilifanikiwa kwa mzee Mkata kumpatia Mbaraka pete hiyo kuku Mbaraka akijua
imetoka kwa baba yake. Wakati Bahati akiyafanya yote hayo, Mzee Mkata hakuwa
akimhoji sana Bahati kwani alielewa maradhi ya aibu yamemtawala sana binti
huyo.
SURA YA NNE
Mwezi mmoja baadae Mbaraka aliondoka
kijijini na kuelekea Dar es alaam ambako ndiko alienda kuendelea na masomo yake
ya chuo kikuu.
Maisha ya mjini alianza kuyazoea na mafanikio
katika masomo yake yalizidi kutokana na jitihada zake.
Walimu wa chuoni hapo takribani wote walielewa
juhudi yake na heshima yake pia.Walimpenda na kumjali sana kwa kila hali.
Alielewa vyema umaskini unaokabili familia
yake na kuelewakwamba yeye ndio suluhisho la kuikomboa familia
yake.Anasa hakuipa nafasi kama ambavyo marafiki zake Josef na Peter walivyokuwa
wakimshawishi na kumsifia maisha ya anasa ili ajiingize katika hayo.
Maisha
ya chuo hicho yalikuwa yametawaliwa na starehe.Wanafunzi wakike walijiuza kana
kwamba wapo kwenye madanguro ya machangudoa wa mitaani.Vitendo viovu kama vile
wizi nao pia ulitawala kwa kiasi kikubwa.
Maingiliano ya kimapenzi na vitendo vya kusagana
kwa waschana viliokuwepo.Yote hayo aliyapa kichogo na kuelewa vyema nini
ambacho kimemleta chuoni hapo.
Ilikuwa ni siku
ya jumamosi majira ya saa 11 jioni, upepo mzuri uliokua ukitoka mashariki
kuelekea magharibi ukipepea na kuisafisha anga ya dunia.
Mbaraka alikuwa pembeni mwa bustani nzuri ya
chuo hicho akiendelea kujisomea kama desturi yake.Baada ya muda kidogo aliskia
sauti ya kike itokayo nyuma yake ikisema
“Mbaraka… Mbaraka…wewe unapenda kusoma!!!”.
Kwa
Ghafla Mbaraka aligeuka nyuma ili kuona ni nani aliekua akimuongelesha.Hakuwa
mwengine alikuwa ni Rehema mtoto wa tajiri mkubwa sana Dar es salaam.
Ni mwanamke
alieumbika kwa sifa zote anazostahiki kuwa nazo mwanamke mrembo.Alikuwa mweupe
mwenye rangi yakuvutia na mwenye asili ya kabila la warangi kutoka Kondoa.Kila
kiungo chake kilikaa mahala pake na kumpendezesha,umtoe kasoro gani mrembo
huyu.Miguu yake minene ya wastani ilimfanya aweze kutembea kwa tambo la kike
huku akimega hatua utadhani anaiyonea huruma ardhi ya mwenyezi Mungu.Binti huyu
hata umpe nguo ya aina gani ilimpendeza na kumvutia kwa kila aliyemtia machoni.Kwakweli
alikua ni chakula cha macho ya wanaume.Wengi walimtongoza na kuambulia patupu.Alikuwa
mkarimu na mpole mwenye sauti nyembamba yenye kuleta mwamkokwa rijali wa kiume.
Ghafla
baada ya macho yao kukutana Rehema alionesha kutabasamu na kuonesha mwanya wake
uliochongeka mithili ya umbo la pembe nne.
Naye Mbaraka hakusita kutabasamu ili kuonesha kutokuchukizwa
na kitendo hicho.Rehema alisogea karibu na kusimama mbele ya Mbaraka mithili ya
mlima wa Kilimanjaro.
“Habari yako Mbaraka Mkata, naona
umetulia peke yako unapiga msuli zaidi” Rehema alimsalimia Mbaraka nakumuuliza
hayo.
“Safi tu sijui wewe” Mbaraka alijibu
“Samahani naweza kujumuika pamoja nawe..?”
Mbaraka
alitabasamu kwa mara ya pili na kuonesha vishimo vilivyochimbika katika mashavu
yake yaliyoanza kuchipua ndevu kwa mbali kisha alimjibu “bila shaka karibu, unapenda
utani Rehema…ulinishtua unajua”.
Rehema alicheka kidogo na kumuuliza “kwanini
ulikuwa mwepesi wa kushtuka kiasi chote hicho, unakua muoga sana”
“Hahaha...kwasababu ulikuja ghafla, istoshe
nyuma ya mgongo siwezi kukuona” alijibu Mbaraka
“Nisamehe mwaya kwa kukushtua na pia
unisamehe kwa kukukatisha shughuli yako ya kujisomea”.Rehema alimwambia
Mbaraka.
Mbaraka hakujali na akamwambia nayeye asijali
pia.Rehema alishkuru kwa hilo.
Kimya
kikubwa kilitawala kati yao kwa sekunde chache, baada ya muda Rehema alishusha
pumzi ndefu zenye nguvu na zilizojaa woga ndani yake.
“Kwanini
unapenda kukaa eneo hili kila wikiend, istoshe ukiwa peke yako…?”. Rehema
alimuuliza
Mbaraka alitabasamu kisha akamuuliza
“Ulijuaje
wewe ?”
“Nilijua
kwasababu nakua nakuona sana istoshe hata mimi pia nakua napenda kukaa paleee…sio
mbali na hapa” huku akimuoteza kwa kutumia kidole chake kilichopambwa kwa rangi
ya kucha ya zambarau.
“Basi inaonesha macho yako yananguvu
sana na upeo wake wakuona mbali ni mkubwa” Aliogea Mbaraka.
Baada ya kuskia hivyo Rehema alitabasamu na
kumwambia “sio sana unanionea tu”. Walijikuta wanafurahi wote kwa kicheko.Waliongea
mengi na kufurahi.
Baada ya muda Rehema aliomba kumuuliza swali.Naye
Mbaraka hakusita kumkaribisha kwa hilo.“Asante” Alijibu Rehema.
“Unatokea wapi, namaanisha familia yako iko
wapi?”
Swali hilo kwa kiasi fulani lilikuwa gumu kwa
Mbaraka kwani kila akiwaza kuhusu kwao hujawa na huzuni ndani ya moyo wake,hii
ni kutokana na hali ngumu ya maisha inayoikabili familia yake,na wala hakupenda
hata siku moja atokezee mtu amuulize kuhusu familia yake kwani kila siku
zikiendelea kusonga familia yake inazidi kuwa katika hali mbaya ya maisha.
Ghafla sura ya tabasamu aliyokuwa nalo liliondoka
kwa haraka utadhani sio yeye alietoka kufurahi na Rehema muda mchache uliopita.
Hali hiyo ilimshangaza sana Rehema na kumfanya ajiulize maswali mengi kwani
alijua kwamba yeye ndio atakua sababu ya kupeperusha furaha ya Mbaraka kwa muda
mfupi.Aliyahisi mabadiliko ya ghafla yaliyojitokeza hivyo hakusita kumuuliza.“Mbaraka
nimekuudhi…mbona umekua tofauti ghafla?”
“Hapana Rehema daima mitihani ya Mungu haiwezi
kumuudhi mwanadamu mwenye kumwamini Mungu mwenyewe” alijibu Mbaraka.
Rehema alishtuka kuskia maneno hayo “Kwanini
unaongea hivyo ” aliuliza Rehema
Mbaraka alichukua sekunde chache bila ya
kuongea chochote kisha akasema “ndio kwasababu hujaniudhi Rehema niko sawa ila
ni mitihani ya Mungu isiyoweza kupingika”.Baada ya kuongea hivyo Mbaraka
alimuomba Rehema wasitishe mazungumzo kwasababu anataka awahi kipindi cha ziada
na muda ulikua tayari umewadia. Rehema kwa kinyongo cha kutoridhika alimkubalia
na kumtaka wakutane tena kesho muda kama huu eneo lile lile.Mbaraka hakukataa kwani
tabia yake ya kumjali na kumuheshimu kila mtu aliendelea nayo kila alipokwenda.
“Haraka haraka haina Baraka” hivyo ndio moyo
wa Rehema ulivyojisemea kimyakimya.
Usiku
wa siku hiyo Mbaraka hakuwa vizuri kimawazo.Akiwa kitandani kwake alikuwa
anawaza mengi sana.Alianza kufikiria shida zinazowakabili wazazi wake kijijini.
Alitambua kwamba yeye ndio tegemeo pekee
katika kuleta furaha ya maisha bora nyumbani kwao.Hakua na jinsi zaidi ya
kuamua kutoa shilingi laki mbili kutoka katika fedha alizodhaminiwa na serikali
ili kesho aweze kuzituma fedha hizo nyumbani kwao. Aliamini kiasi hicho cha
fedha kingeweza kuwasaidia kwa kiasi fulani wazazi wake.Fedha ambazo amepata
kudhaminiwa na serikali hazikuwa zinakidhi haja ipasavyo ila hakua na jinsi
kufanya hivyo.
SURA YA TANO
Juampili asubuhi Mbaraka aliamua kuamka mapema ili ajitaarishe
apate kumuwahi mtu ambae atweza kumkabidhi fedha hizo azifikishe nyumbani.
Kiukweli Mbaraka alikuwa ni mwanaume mrembo
sana.Wazungu wanasema handsome boy.Kila siku zilivyokuwa zinazidi kusonga
alizidi kuvutia kwa wasichana kwa kila sifa ya uwanaume.Siku ya leo aliamua
kutoka kiaina.Alivaa suruali aina ya
jinzi iliyokuwa na alama za kuchanika kutoka China,juu alitupia flana
nyeusi iliyokuwa nyepesi kiasi cha kuonesha maumbile ya kifua chake
kilichojazia. Ilikuwa ni flana yenye mng’aro na yenye picha ya msanii maarufu
aliyependwa sana huko Jamaika.Miguuni alivaa viatu aina raba nyeupe na mistari meusi.Kiukweli
alipendeza sana utadhani alikuwa ni mwanamitindo kutoka ulaya.Mkononi alivaa
saa aina ya saiko yenye mng’aro wa rangi ya dhahabu na yenye kumeremeta
kutokana na rangi yake.Baada ya hapo alijipulizia mafuta yenye kunukia vizuri
aina ya ESCADA.
Alianza kuteremka ngazi kutoka chumbani akiwa
anaharakia katika jukumu la kutuma pesa nyumbani kwao,ghafla akiwa anashuka
ngazi kutokana na haraka zake alijikuta anagongana na Rehema kwa bahati mbaya.Rehema
aligeuka kwa ghazabu baada ya kupata
maumivu makali mgongoni kwake,lakini ghadhabu zake ziligeuka na kuwa furaha
baada ya kuona kwamba alikua ni mwanaume anayempenda sana ndie aliemgonga kwa
bahati mbaya.
Mbaraka
alikuwa mnyonge kwa kitendo kile, alikuwa amesimama kama mgambo aliekuwa katika
kazi yake ya lindo la usiku, hakujua aanzie wapi ili aonekane mkweli kwamba
hakuwa amekusudia kumgonga.Rehema alikwishajua kwamba hakuwa amekusudia.
Baada
ya Rehema kugeuka vyema alishangaa sana kumuona Mbaraka katika muonekano mzuri
ambao hajawahi kumuona nao tangia kuanza kumfahamu. Hakuweza kuamini macho
yake, alitamani amrukie na amkumbatie kifuani kwake lakini hakuweze kufanya
hivyo kutokana na pisha pisha za wanafunzi wengi eneo lile.
“Mbaraka
ni wewe lakini?” Rehema alimuliza
“ni mimi Rehema,samahani sana sikukusudia kufanya hichi kilichotokea hapa bali
yote ni kutokana na haraka zangu na mawazo yasiyoisha kichwani mwangu…”.
Rehema hakujali kilichotokea nae alimtaka asijali
pia.
Alimuuliza“kwanini
umekuwa na haraka kiasi hicho unaharakia nini?”
Kiukweli lilikuwa ni swali lililomchanganya
Mbaraka kwasababu lilikuwa rahisi lakini lenye uzito wa kujibu kiupande wake, lakini
hakuona kama itakuwa vyema akimficha Rehema ambae alimthaminin kwa kumuuliza
hivyo kwa bashasha ya kutaka kujua.
Mbaraka
aliishinda nafsi na aliona wacha tu amwambie anaelekea sehemu gani, alimjibu “Naelekea
ubungo kwasababu nahitaji kumfikishia mtu huu mfuko nilioushika hapa, nae
anaenda nyumbani ili aufikishe kwa wazee”
Rehema
alitabasamu kwani aliona Mbaraka ameanza kumjali sasa.Hakuweza kuelewa ni nini
kilichokua ndani ya mfuko ambacho kilikuwa kinaharakishwa namna hiyo. Hakutaka
kuliacha nyuma, aliuliza akiwa amesimama kwa kutumia vidole vya miguu yake, wakati
huo mikono yake ameiweka juu ya mdomo wake,
“Tunaweza kwenda wote …,I mean kukusindikiza...?”
aliuza Rehema.
Mbaraka
kwa vile alikuwa anachelewa sana na kuhofia kumkosa mtu ambae aliahidiana
nae,hakutaka malumbano na maongezi yaendelee zaidi,aliamua kukubali kuongozana
nae.Rehema alifurahi sana.
Wakati
wanaharakia kutoka nje ili wawahi, mawazo yao ya kupanda gari yalikuwa
yanapingana. Kwani mawazo ya Mbaraka yaliwaza kuwahi gari abiria,wakati Rehema
aliwaza ni jinsi gani ataweza kuendesha gari kwa haraka ili kumuwahisha
Mbaraka.Kilichomshangaza Mbaraka ni kuona kwamba Rehema alichapuka zaidi yake
huku akiwa ameielekea gari aina ya RANGE ROVER yenye rangi nyeusi inayong’aa ambayo
ilikuwa imepaki pembeni ya geti la kutokea nje ya chuo.
Mbaraka
alishangaa sana na kilichompa mshangao zaidi
ni kuona mkono wa kushoto wa Rehema umeshika na kuning’iniza funguo.Moyo
wake ulishtuka na kushangaa kiasi cha kuanza kujiuliza maswali moyoni mwake
“hivi ile gari ni ya Rehema au nipo ndotoni”. Moyo wake ulishindwa kujibu swali
hilo ispokuwa alipata jawabu baada ya Rehema kufika karibu na kuingia ndani ya
gari ile akimsubiria yeye afike ili waondoke.
Mbaraka hakuweza kuamini kilichotokea kwani kwa kipindi chote
alichozoeana na Rehema hakuweza kuelewa
kama anaweza kumiliki gari kama hilo
amabalo yeye aliishia kuliona likiendeshwa na watu maarufu sana na wenye
utajiri mkubwa. Alihisi kama ndoto za usiku zinamjia wakati tayari alishaamka.
Kwa haraka Rehema alifungua kioo cha gari na
kumuashiria Mbaraka apite mlango wa pili.Mbaraka alielewa lugha ya ishara iliyotumiwa na Rehema,kwa
haraka alizunguka upande wa pili na kufungua
mlango na kuingia ndani.
Kumbe urembo wa Rehema haukuwa katika
muonekano wa mavazi tu bali hata anapokaa popote alipendeza.Ndani ya gari lake mulikuwa
musafi na harufu ya aina yake.
Aliwasha
gari lake na kutoka nje.Alimuuliza Mbaraka “kwaio ndio tunaeleka ubungo?’
“Ndio,na muda tulioahidiana na huyo mtu ndio
huu unakaribia,nataka nimpatie pesa azifikishe nyumbani” alijibu Mbaraka.
“Nakama
hatukumuwahi huyo mtu unaemtegemea basi tatuma kwa kutumia njia nyengine”aliongeza
Rehema huku akianza kuingia barabarani.
Alikuwa akiendesha gari kwa uzoefu na kwa
umakini mkubwa,waakati huo Mbaraka alikuwa akimuangalia sana Rehema jinsi
alivyokuwa anamiliki gari vizuri akiwa njiani.Alitamani hata siku moja nayeye
awe anamiliki gari japo sio kama ya Rehema.
Kwa dakika chache waliwasili stendi ya mabasi
ya mikoa na kufanikiwa kuingia hadi
ndani ya stendi hiyo.Mbaraka alitia mkono mfukoni na kutoa simu aina ya
Nokia ya tochi.Alianza kuanza kubofya.Punde tu baada ya kubofya simu hiyo alionekana
kijana akichapuka kumfuata Mbaraka pale alipokua amesimama. Rehema alimuona mtu
huyo akija kwa kasi lakini hakuweza kujua kwamba ndie ambae ameahidiana na Mbaraka
kumkabidhi mzigo.Alifika na kusimama mbele ya Mbaraka
“Mambo vipi Mbaraka, samahani sana kwa
kukusumubua,maana nahisi nimechelewa”,alisema mtu yule aliyekuwa mrefu sana.
“aahh!!!,hapana
ila mimi ndio nimekusumbua sana na nataka nikusumbue zaidi…” Mbaraka alimjibu na
kuendelea kumwambia kwamba“mzigo wenyewe ni huu (huku akimuonesha mfuko mweusi
aliokuwa ameushika mkononi), nataka unifikishie kwa mzee Mkata”
Yule
mtu alianza kunywea kwani gari lilikuwa limeshaondoka na hata yeye alipofika
stendi hakuliwahi.Hakuwa na jinsi kumueleza ukweli na kumtaka amsamehe kwa
kumsumbua.
Kwa
vile urafiki wa kweli haupotei Mbaraka aliahidi kumsamehe na kumtaka asijali
kwani alikuwa anajuwa njia gani nyengine ya kutumia ili mzigo ule ufike kwa
haraka.Waliagana hapo.
Wakati
wote huo Rehema alikua amesimama na kutazama kilichokua kinaendelea.Alijiskia
furaha kubwa kuwa na Mbaraka kila wakati.Mawazo yake wakati huo yalimpeleka mbali
na kuhisi kwamba tayari wameshakuwa wapenzi.Mbaraka na Rehema walirudi ndani ya gari yao na yule mtu kuelekea upande wa pili.
Wakiwa
ndani ya gari Rehema alimuangalia Mbaraka usoni na kugundua kuwa hakuna furaha
ya aina yoyote ndani ya moyo wake.Kwa vile Rehema alimpenda sana Mbaraka na
alipenda kila wakati amuone akiwa na furaha alimtaka waelekee katika kituo cha
tigo pesa ili amsaidie fedha hizo kufika nyumbani kwa haraka.
Mbaraka hakulipinga hilo na alianza kuonesha
uso wa tabasamu.Rehema aliwasha gari yake na kuelekea katika kituo cha karibu
anachokielewa Walifika Manzese mtaa wa Argentina ndipo walishuka gari na
kusogea karibu na kituo cha tigo pesa. Rehema alimtaka Mbaraka afanye
mawasiliano na watu wa nyumbani kwao kwa kuwapa taarifa kwamba atatumia njia
hiyo na hela zitawafika kwa kupitia mtu ambae Mbaraka alimuelewa. Hakusita
kufanya hivyo kwa dakika chache na ndipo alimtaka Rehema afanye mambo yake
kwasababu yeye alikuwa haelewi chochote kuhusu utaalamu huo licha yakukaa mjini
kwa muda mrefu, kwani hakuwahi kumtumia mtu yoyote pesa kwa njia hiyo.
Alifungua mfuko aliokuwa ameushika mkononi na
kutoa kiasi cha fedha kilichokuwemo ambacho ni shilingi elfu tisiini za
kitanzania, alimkabidhi Rehema, bila hofu.
Kwa
ghafla Rehema alionekana kushangaa sana baada ya kuhesabu fedha hizo.Mbaraka
aliuliza, “mbona hutumi sasa na fedha nimeshakupatia …?” Rehema alishangazwa sana
na kiasi hicho kidogo cha fedha ambacho Mbaraka anasumbuka tangia asubuhi
kutaka kutuma fedha hizo.Yeye alidhania fedha hizo ni nyingi sana zisizopungua
milioni moja, hakuweza kustahamili aliamua kumuuliza kama ambae hakuelewa
chochote “ndio hizi, mbona ni chache sana...?”
Mbaraka
hakupenda kuulizwa swali hilo kwasababu hakuwa anapenda iwe hivyo,alipenda
kutuma fedha nyingi sana ili aweze kuwatunza wazazi wake kwa kiwango kinachokidhi
mahitaji yao lakini hakuwa na uwezo huo.Alitamani amiliki mamilioni ya fedha
ila zilibaki kama ndoto kichwani mwake,jitihada zake zilifikia elfu tisiini tu.
“Usijali Rehema,naomba uzitume hizohizo,then
siku nyengine nitakuja kuwatumia tena zaidi”.Mbaraka aliyaongea hayo akiwa
katika hali ya huzuni sana,hakupenda mtu yoyote agusie kuhusu familia
yake,kwani alikua anaumizwa sana na mateso ya umaskini nyumbani kwao,lakini pia
hakuweza kumlaumu Rehema wala kumkasirikia kwasababu aliamini kua Rehema hakua
anaelewa chochote kuhusu ugumu wa maisha yake.
Kutokana
na hali ile Rehema aligundua ukweli kwamba Mbaraka hakuwa na fedha na ndio mana
amelazimika kutuma kiasi hicho cha fedha kwani aliamini kwamba hakuna
asiyependa kuifaidisha familia yake, wala hakuna anaependa kuiona familia yake
ikiteseka kwa shida za kimaisha.Kwa mbali sasa alianza kuelewa kwamba Mbaraka
hakua na hali mzuri kimaisha.
Baada ya kujibiwa hivyo hakuweza kutuma fedha
zile,aligeuka nyuma na kuingia ndani ya
gari,baada ya sekunde chache alitoka akiwa ameshikilia kiasi cha fedha
zisizopungua laki saba na kumtaka mhudumu atume laki saba badala ya elfu
tisiiini.
Mbaraka alishangazwa na kitendo kile,hakuelewakwanini
Rehema anaamua kufanya vile.
“Kwanini unaamua kufanya hivyo” Mbaraka
alimuuliza.
“Kwanini nawe umeniuliza hivyo au hupendi pesa
zangu ziende kwenu...?” nae Rehema alimuliza kabla yakumjibu swali lake.
Mbaraka
alimtaka samahani kisha alitia mkono mfukoni na kutoa karatasi iliyoandikwa
nambari za simu na kumpa mhudumu.
“Tuma
kwenda namba hii”. Alimwambia mhudumu.
Baada ya dakika mbili mhudumu alimwambia
tayari ameshafanya hivyo,na aliwashukuru sana na kuwakaribisha vyema.Rehema
hakuwa nyuma nae aliitika vyema na kumshukuru mhudumu kwa sana.Waliingia kwenye
gari yao na kuanza kuondoka.Wakiwa njiani Rehema alimtaka Mbaraka afanye
mawasiliano na nyumbani ili kuwataarifu kuwa fedha zimeshatumwa. Mbaraka
hakusita kufanya hivyo.
Kwawakati
ule Mbaraka alikuwa na furaha isiyomfano, kwani alitamani amkumbatie Rehema na
kumshukuru kwa alilolifanya.Alihisi kama tu akimwambia ahsante haitoshi na
ndipo aliamua kumuuliza “Rehema nikupe shukrani gani mana asante pekee
haitoshi”
Rehema alitabasamu kidogo kisha akasema “hivi mbaraka
kwanini unataka unishkuru mimi?, nivyema ukimshukuru Mungu ambae ndie
anaestahili kushukuriwa,kwani yeye ndio ameniwezesha mimi kufanya haya”.
Mbaraka alihisi kama amechanganyikiwa.
“Shukrani
zinastahiki na kwako pia, wakati Mungu nilishamtanguliza mwanzo”alijibu
Mbaraka.
Rehema
alifurahi sana kuskia maneno hayo kutoka kwa Mbaraka.
Kwa vile muda ulishaenda sana na majira ya saa
saba yalishakaribia Rehema bila kuongea chochote tena kuhusu shukrani alimtaka
Mbaraka waende kupata chakula cha mchana katika restaurant moja maarufu sana iliyopo
maeneo ya Sinza afrika sana.
“Daima mtaji wa maskini ni nguvu zake mwenyewe” Mbaraka alikubali wazo la Rehema bila
kipingamizi.
Walifika eneo hilo na walikula chakula cha
mchana.Baada ya kumaliza Mbaraka alimshukuru sana Rehema kwa wema wake ambao
amemfanyia tangia asubuhi. Kiukweli Mbaraka alishaanza kuelewa sababu ya yote
hayo anayoyafanya Rehema.
“Mapenzi
tu ndio yanayomfanya afanye yote hayo” kauli hiyo ilipita kichani mwa Mbaraka
mara kwa mara.
Rehema
alimwambia Mbaraka kwamba
hajiskii kukaa chuo kwa leo
kutokana na machofu pamoja na kichwa kuanza kumsumbua,hivyo alimtaka
amrudishe yeye tu halafu mwenyewe atarudi nyumbani.Baada ya kuambiwa maneno
hayo Mbaraka hakuonesha uso wa furaha kwani alimzoea kwa muda mchache tu.
Kwavile hakuwa na uwezo wa kumponesha
alimtakia pole na alimshauri ameze dawa za maumivu ndipo
aende nyumbani.Rehema alifurahi baada ya kuambiwa ameze dawa kwanza, kwani
aliona sasa kumbe na mwenzake naye
anamthamini sana na anathamini uwepo wake.
Rehema alikuwa anajali sana afya yake, alipenda
kutembea na dawa kama hakiba katika gari lake la kifahari.Alienda kununua maji
katika duka lililokuwepo karibu yao ndipo waliingia ndani ya gari na Rehema kumeza
dawa na kuanza kuondoka.
Wakati walipoanza kukaribia kufika chuo Mbaraka
alimwambia Rehema “unajiskiaje sasa?”, huku akimuangalia
“afadhali,nashkuru sana Mbaraka kwa
kuonesha kunithamini…” Rehema alijibu kwa furaha.
Mbaraka alitabasamu kisha akamuuliza tena “kwani
nimekuthamini kitu gani Rehema kinachouzidi wema wako”,
“Kujali afya yangu inazidi thamani
nilokuthamini mimi” Rehema alijibu akiwa na bashasha sana moyoni mwake.Mbaraka
alifurahi sana.
Walifika nje cha chuo Mbaraka alishika mlango
wa gari kutaka kutoka,ghafla Rehema alishindwa
kuvumilia,na kuamua kushika bega la Mbaraka.Mbaraka alisita kutoka na
kugeuza kichwa chake nyuma kumwangalia Rehema pengine huenda kuna kitu
amesahau.Uso wa mrembo Rehema ulikuwa ni wenye huzuni sana,alionesha ishara ya
kuwa hawezi kukaa mbali na Mbaraka,alitamani hata amchukue nyumbani kwao ila ni
jambo lisilowezekana kwasasa.
Moyo wake ulishamchagua zamani Mbaraka na
anafanya haya yote kwasababu ya mapenzi.Rehema alionesha huruma sana.Aliamua
kumuachia Mbaraka na kumsindikiza kwa neno lilompa Mbaraka mawazo muda wote.
“Karibu Mbaraka. Laiti ungekuwa wewe ungeumia
zaidi.”Hayo ni maneno ambayo Rehema alimwambia Mbaraka wakati anataka kutoka
ndani ya gari.
Mbaraka alishindwa kuongea chochote na alibaki
kumuangalia Rehema usoni.Nyuso zao wote zilionekana kutoridhika kwa kila mmoja
kukaa mbali na mwenzake,ndipo aliamua kufungua mlango wa gari na kumuaga kwa
ishara ya mkono uliomaanisha kwaheri Mungu
akupe pole.Rehema alitabasamu na kuamua kuwasha gari na kuondoka.
SURA YA SITA
Usiku
wa siku ile Mbaraka hakuweza kupata usingizi hata chembe,muda wote aliutumia
kuyawaza maneno ya Rehema aliyomwambia wakati alipokuwa anashuka gari.Mawazo
yaliuzidi nguvu moyo na ubongo wake.Hakuwa anapenda kumuona mtu aliyemthamini
kwa kiasi kikubwa anaumia kwa lolote lile,alijiuliza maswali yaliyomshinda
kupata majibu yake.Hakuweza tena kuvumilia,usiku ule aliamua kumuamsha rafiki
yake wa karibu aliyekuwa amelala kitanda juu ili aweze kumsaidia katika hili.Baada
ya kumuhadisia kila kitu Rashidi alisikitishwa sana na habari hiyo,alihisi kama
Mbaraka anamtesa Rehema kwa makusudi kutokana na alivyomueleza kila kitu
Rashidi alijua fika kwamba hakuna sababu inayomfanya Rehema ayafanye yote hayo
zaidi ya mapenzi.Rashid alikua mtoto wa mjini kama akina Piter na mwenzake, lakini
yeye hakua anapenda anasa na ndio maana Mbaraka alimuamini na kumsimulia yote. Alimpa
ushauri kwa kumtaka muda huo huo ampigie simu ili kumliwaza kwani ni dhahiri
atakua anateseka kwa mapenzi juu yake.Mbaraka alimshukuru sana Rashidi na
alimuomba samahani kwa kumsumbua usiku mnene, alimtaka aendelee kupumzika.
Kwa
vile Rashid alikua ni rafiki mwema kwa mwenzake nae hakulijali hilo.
“Bila samahani ila fanya ivyo
nilivyokuambia” Rashid alimjibu rafiki yake na akaendelea kulala.
Mbaraka hakuweza kuamini kwa asilimia zote
maneno ya Rashidi kwamba Rehema atakua anampenda, kwani yeye aliamini kwamba
atakua anayafanya yote kwa ubinaadamu tu na istoshe alishatambua kwamaba Rehema
ni binti wa kitajiri hawezi kumchagua maskini kama yeye asie na chochote zaidi ya
dhiki na hali ngumu ya maisha.Hapo mawazo yalimzidi sana na alihisi kama Rashidi
ndio amabae amezidi kumchanganya.
Licha ya kutokuamini moja kwa moja maneno ya
rafiki yake lakini aliamua kufanya kama alivyoshauriwa kwamba ampigie simu Rehema
kwani atakuwa anateseka sana kwaa ajili yake.
Kumbe maneno ya Rashidi hayakuwa yameenda
upande kwani wakati wote huo naye Rehema hakuwa katika usingizi zaidi ya
kumuawaza Mbaraka kwa kila hali.Alikua anaumia sana ila hakua na lakufanya
zaidi ya kuwaza kwamba pindi atapoamua kumwambia ukweli asingemfikiria kwamba
yeye ni Malaya.
ALIJIULIZA
sana hilo. Hakujua Wapi aanzie na pia aligundua kwamba iwapo atajinyamazia
kimya na kuyalimbikiza moyoni basi yangemuumiza moyo wake na pia ataweza kuandamwa
na ugonjwa wa mapenzi utaosababisha hata kupoteza dira katika masomo yake. Aliwaza
na kuwazua,ila alikumbuka kwamba haraka haraka haina haraka hivyo alihisi ni
bora asiliharakie hili.
Kila
alipojaribu kulitoa akilini ilimuwia ugumu sana kwani moyo wake ulishapenda.
Ghafla alikumbuka msemo usemao kwamba “ngoja ngoja yaumiza matumbo”. Aliamua
kukamata simu yake aliyokuwa ameiweka chini ya mto wa kulalia na kuanza kuipiga
simu ya Mbaraka.Wakati alivyokua akijaribu kuipiga ilikuwa inakata njiani kana
kwamba ilikuwa busy.Tukio hilo lilizidi kumuumiza moyo wake kwani alihisi kwamba kukatika kwa simu hiyo
hakukua na sababu nyengine zaidi ya
Mbaraka alikuwa bize na wanawake wengine.
Usilolijua
ni sawa na usiku wa kiza kwani wakati huo nae Mbaraka alikuwa anapiga simu ya
Rehema nayo ilikuwa inakata njiani.
Mbaraka aliamua kuwacha simu ili apumzike kama
angeweza kupata usingizi. Rehema hakuchoka kujaribu kuipiga tena simu ya Mbaraka
na ndipo kwa mara ya mwisho simu iliita. Mbaraka alifurahi moyoni baada ya
kuona kuwa ni Rehema ndie aliekuwa akipiga simu usiku ule. Aliipokea lakini kabla
ya yote alitaka kujua anaendeleaje na kichwa kilichokuwa kikimsumbua mchana.Rehema
alifurahi kuulizwa hivyo “asante my, naendelea vizuri punde tu baada ya kusikia
sauti yako” Rehema alijibu akiwa na faraja moyoni mwake.
Mbaraka
alitabasamu baada ya kusikia hivyo, kisha akamwambia “ha ha ha…alafu wewe
unapenda uchokozi sana,hivi kwanini sauti yangu iwe ndio dawa yako?”
Rehema hakutaka kuficha chochote na aliona
huo ndio muda pekee wakulifikisha lile lililomo moyoni mwake kuliko kufuga
maumivu ambayo yataweza kumuumiza kila wakati.
“ Kwasababu moyo wangu umekuhifadhi
wewe na wewe na ndio mana ninapoumwa jua
furaha yangu imepotea moyoni,ila sauti yako ndio imerudisha furaha hiyo
kwasababu ni wewe pekee ambae upo moyoni mwangu” Rehema alijibu bila aibu,kwani hakutaka
tena kuficha maradhi yake mbele ya daktari bingwa.
Sasa Mbaraka alianza kuyaamini yale maneno
aliyotoka kuambiwa na rafiki yake.Mbaraka alifurahi sana.
“ kwanini
mpaka muda huu hujala?” Aliuliza Mbaraka
“kwasababu
kuwepo mbali kwako ndiyo sababu inayonifanya nikose usingizi,na ndio maana
nimekupigia wewe ili unipenusingizi wangu” alijibu Rehema.
Kwavile alikua ni binti wa mjini hakushindwa na lakusema
kwani mjini daima kuna mengi.
Mbaraka
alianza kushangaa na kuhisi kwamba maneno yale
hayakuwa yanatoka moyoni mwa Mehema labda alikuwa na kitabu kilichoandikwa
hayo pembeni. “asante Rehema,nimefrahi kuskia hivyo lakini naomba nikulize
kitu”
“Bila shaka, uliza tu” alijibu Rehema.
“Kwanini uliamua kunizuia pale nilijaribu
kuteremka gari na kuonesha kutoridhika na kitu Fulani?”.
Swali hilo lilikuwa zito sana kwa Rehema kwani
jawabu lake ndio lilikuwa kiini cha thamani yote aliyokuwa akimuonesha,aliamua
kukaa kimya kwa sekunde chache. Mbaraka
alihisi anaongea peke yake,aliamua kumwita ili aamini uwepo wake kwa wakati
ule.Rehema aliitika na kumwambia “naomba unisamehe Mbaraka kwani jawabu la swali
lako hili litaweza kukuudhi na inawezekana hutotaka tena kuniona katika upeo wa
macho yako,naomba usije ukanifkiria tofauti kwa kuongea ukweli uliomo
ndani ya moyo wangu...”
alivuta pumzi kidogo kisha akaendelea,“ukweli
nikwamba nakupenda sana na nahitaji uwe
dira njema katika maisha yangu,nilianza
kuteseka juu yako kwa kipindi kirefu sana na nilistahamili maumivu ila sasa
nimeshindwa na ndio maana nilikwambia naumia sana na maumivu yangu yataondoka
pale tu utakapotamka kutoka moyoni mwako kama unanipenda,nisamehe Mbaraka kwani
nilihisi kama ulikua unanionea na kuzidi kuniumiza kwasababu nilikuonesha
ishara nyingi kwamba tayari ulishakuwa umehifadhiwa moyoni mwangu...” Rehema alianza kujawa na huzuni kila
alipozidi kuongea.
Nae Mbaraka
alianza kutowa na machozi na kuhisi kwamba kumbe angeweza kumpoteza mtu muhimu
sana katika maisha yake,hakuwa aliyeelewa chochote kuhusu ishara hizo na alimtaka
Rehema asiongee mengi kwani machozi
yalikua yameshafika mashavuni mwake na angezidi kumzidishia huzuni.Alimwambia “naomba unisamehe sana Rehema,katika kipindi
chote hicho mimi sikuweza kuelewa chochote
kuhusu moyo wako,na kwanini usingechukuwa uamuzi huo zamani tu wakuniambia?,am
sorry Rehema naomba tuongee kesho sasa hivi muda umeenda sana,na istoshe mimi nalala na wenzangu humu,hivyo
haitapendeza wakiyaskia haya”. Rehema alihisi anaonewa kwa kucheleweshwa kujua ukweli ila alimuelewa Mbaraka
na kumwambia “bila shaka,ila kesho wazazi wangu watakuwa na ziara nje ya nchi
kwahivyo nakuomba tuwe pamoja nyumbani nadhani
tutaweza kuongea vizuri.Naomba unithamini Mbaraka kama ninavyokuthamini
na unijali pia,nadhani inaweza kupunguza maumivu ya moyo wangu”.
Mbaraka
hakupendelea sana kuenda sehemu asipojulikana,ila angefanyaje na hataki
kumuumiza mtu aliyejitolea kumthamini.
Alimuahidi
kuwa watakuwa pamoja.Rehema alitabasamu na kukata simuhuku akitamani kukuche
ili aweze kuwa pamoja na ampendae.
SURA YA SABA
Asubuhi
ilipofika Rehema akiwa ndani ya jumba
lao la kifahari,alikua wakwanza kuamka na kufanya usafi kama ilivyo desturi
yake awapo nyumbani.Baada ya muda mfupi na wazazi wake pia waliamka kwa lengo
la kujiandaa na safari kwani haikuwa ni safari ya karibu. Hata ilipotimu saa
mbili kamili Rehema alikuwa tayari ameshawaandalia wazazi wake chai na
kuwahimiza kuwahi mapema. Aliwaharakisha makusudi ili awe mkweli juu ya ahadi
aliyoahidiana na Mbaraka. Wazazi wake
hawakuwa wavivu juu ya hilo, wote walijitahidi kuwahi mezani wakiwa
wameshajiandaa kwa kila kitu.
Bila ya kupoteza muda walipata chai iliyokuwa
imeandaliwa vyema na mtoto wao.Walimaliza na kumtaka Rehema awasindikize ili
kusudi aweze kurudi na gari nyumbani.
Majira ya saa tatu na robo Rehema aliingia
chumbani na kubeba begi lililokuwa limeandaliwa vyema na kusheni nguo ambazo
zitaenda kutumika waendako. Wote waliingia ndani ya gari na walimuamuru Janeth
ambae alikuwa ni mfanyakazi wa ndani afungue geti pindi watakapotoka.
Safari ya kutoka hapo na kuelekea uwanja wa
ndege wa taifa ilianza.Hazikupita dakika nyingi Rehema aliwasili uwanjani na
kuagana na wazazi wake kwa huzuni kwani alikuwa anawapenda sana kama walivyokuwa wanampenda mtoto wao wa
pekee. Lakini hakuhuzunika sana kwasababu haikuwa safari ya milele bali ilikuwa
ni yamuda mchache tu.
Baada ya kuhakikisha ndege imeshaondoka hakuwa
na sababu ya kukaa sana hapo kwani alihitaji kuzidisha uaminifu wake kwa
Mbaraka, aligeuza gari na kuanza safari ya kurudi nyumbani kuonana na yule
anaeutawala moyo wake kwa sasa. Wakati
huo naye Mbaraka alikuwa anajiandaa ili kutimiza ahadi alioisaini usiku wa
jana.Alienda kukoga na kuanza kujitayarisha kwa mavazi mazuri na manukato ya Dubai.
Kwa vile Rehema hakuwa anaishi mbali na chuo basi
nae Mbaraka hakuwa na wasiwasi moyoni mwake kwamba angeweza kuchelewa.Alianza
kujitoa kimtoko. Kilichobaki ni kumuaga rafiki yake kwamba anaenda kuonana na Rehema
nyumbani kwao. Rashidi alimruhusu na kumuachia ziada ya maneno kwamba asije kumuudhi Rehema kwani anampenda sana na
ni Bahati kupendwa na mrembo kama huyo mwenye utajiri mkubwa nyumbani kwao.Mbaraka
alikirii kutofanya hivyo kwani tayari nae ameshaanza kumpenda Rehema.Aliteremka
ngazi na kuelekea nje.Alifika nje ya chuo na kuchukua bodaboda ili jasho lisijekumuharibia
manukato yake.
Rehema
nae punde aliwasili nyumbani huku akitarajia kwamba atakuwa amemuudhi Mbaraka
kutokana na foleni za barabarani zilizomfanya kuchelewa kidogo lakini haikuwa
hivyo kwani Mbaraka alikuwa hajafika kwa wakati huo.
Aliingia chumbani kwake akiwa hana furaha
kwani alijua kwamba maneno ya Mbaraka hayakuwa na ukweli ndani yake.Hakua
amefika mpaka sasa.Aliamua alijitupa kitandani kwa hasira baada ya kuangalia
saa yake ya mkononi iliyomwambia kwamba ni saa nne na dakika 35.
Machozi
yalianza kumtoka.Alijua kwamba Mbaraka hajaweka matumaini ya upendo juu yake, alihisi
uchungu wa moyo na asijue lakufanya.Alishika simu yake ili amtumie ujumbe mfupi
kwa msukumo wa hasira zake na uchungu wake aliokua nao wakati ule.Ghafla
aliskia honi ya pikipiki nje ya nyumba yao,alinyanyuka kutoka kitandani kwa
haraka na kusogea dirishani ili aweze kuona kwamba alikwa yeye au lah.Kutokana
na ukubwa wa nyumba yao hakuweza kuona chochote kilichokuwa nje ya geti.
Aliamua
kutoka chumbani kwa haraka na kukimbilia getini aende kufungua kwani huenda alikuwa ni Mbaraka.
Moyo wake haukumdanganya kwani alifika na
kufungua geti ndipo alipomuona ampendae kwa dhati akiwa anajipangusa mavumbi
kwenye viatu vyake.Ghafla nae Mbaraka alitupa macho yake mlangoni ili kuona
nani alikuwa muhusika wa kufungua mlango huo,haikuwa mategemeo yake kumuona Rehema
akiwa ameshikilia geti huku akimuashiria
kwa macho kwamba kulikuwa na sababu iliyomfanya amwage
machozi,hii ni baada ya kuona ishara ya macho yake kuwa mekundu. Alikuwa na furaha baada ya kumuona
Mbaraka, “karibu nyumbani Mbaraka,nahisi umechoka sana mana umetapakaa mavumbi
sana”,Rehema alisema.
“Asante”,Mbaraka
alimjibu na kumtaka samahani kwa kuchelewa hadi kuyafanya kumfanya macho yako
yafunguke kwa wingi kwa kilio.
Rehema alimuangalia Mbaraka kwa macho ya mahaba
na kumtaka asijali kwa hilo.Mbaraka hakuwa ametuliza kichwa chake tangu aingie
ndani ya jumba hilo,alihisi kama
ameingia ikulu,hakuwa na mfano wa kuifananisha nyumba hiyo kwauzuri na ukubwa
wake.
“Karibu
na ujiskie upo nyumani” Rehema alimkaribisha huku akionekana akiwa na furaha
sana.
Mbaraka
aliketi juu ya sofa la aina yake ambapo tangia kuzaliwa kwake hii ilikuwa ndio
mara yake ya kwanza kuona sofa kama hilo.Alianza kuangaza macho macho yake kama
ambae hakuwa anajielewa yupo sehemu gani.Rehema aliligundua hilo kwa mbaraka na
kumtaka apunguze wahaka hayo ni mambo tu ya kawaida.
Mbaraka alitabasamu na kupumua kidogo huku
akimuangalia Rehema kwa kutokuamini kwamba ipo siku ingeweza kutokea Rehema
kumkaribisha kwao kwa heshima zote.
Wakati
huo Rehema alikuwa ameshughulika kuandaa chai mzuri kwa ajili ya mgeni wake.Ilikuwa
ni chai ya aina yake ambayo haijawahi kuingia katika kinywa cha Mbaraka tangia
kuzaliwa kwake.Aibu haikumuacha mkono.Dakika chache zilipita na Rehema alisogea
mbele ya Mbaraka na kumsimamia kama anamdai deni la muda mrefu ambalo alimgomea
kumlipa.
Alimtaka asogee mezani ili akajipatie chai
iliyoandaliwa kwa ajili yake.Mbaraka alisogea mezani.
Ilikuwa
ni meza kubwa yenye umbo la mviringo iliyotengezwa kwa kutumia kioo kitupu
ambapo ulieweza kuona kila kitu kilichokuwa chini ya meza hiyo.Aliketi juu ya
kiti akiwa na woga kwamba kiti hicho kisingeweza kuhimili uzito wake kutokana
na wembamba wa kiti hicho cha kioo.Ushamba ulimuandama kwa kiasi kikubwa.
Wakati wote huo Rehema alishakaa juu ya kiti
akiwa anamuangalia Mbaraka kutokana na uzuri aliokuwa nao,hakuwa
anaridhika kila alipokuwa akimtazama.
kwa muda mawazo yake yakampeleka mbali na kuhisi kama yupo kitandani na mwanaume huyo. Ghafla aliskia sauti
ikisema “mbona unachelewa?”, haikuwa sauti ya mtu mwengine ila ni Mbaraka baada
ya kuona Rehema yuko mbali kifikra. Aligutuka ghafla na kumwambia“samahani
Mbaraka… niliwaza kitu cha kifamilia hapa mana…nimeanza kumkumbuka sana mama
yangu”.
“Pole
watarudi tu” alijibu Mbaraka.
“Asante...karibu chai Mbaraka jiskie upo
nyumbani wala usione aibu”.
Walianza
kunywa chai huku kila mmoja akimwangalia mwenzake usoni kama kwamba hawajawahi
kuonana hata siku moja katika maisha yao. Mtazamo wa mrembo Rehema ulilenga moja
kwa moja juu ya kilele cha mahaba na alianza kulegeza macho yake.Wakati huo mtazamo wa Mbaraka kwa Rehema ulikuwa ni
wa kutoamini kama ipo siku angeweza kupendwa na mwanamke mrembo kama huyo mwenye kila kitu na asiekuwa na shida zaidi ya
kuzidiwa na raha za kila aina.
“Hongera Rehema kwa chai tamu...kumbe umesomea
mapishi eenhh!!,tena nadhani sio ndani
ya nchi hii…”,Mbaraka alisifu.
“mmhh!!! Unaanza sasa matani yako”, Rehema
alitabasamu na kufurahi kuskia maneno hayo matamu kutoka kwa Mbaraka.
“Napenda sana kupika…na hata nikiwa off days
huwa namsaidia dada wa kazi katika suala la kupika na ndio mana umeridhika na
chakula change, asante”.
SURA YA SABA
Mbaraka alianza kujiskia uhuru sasa, alikunywa
chai na kumwambia Rehema tumbo lake limeshajaa chai tamu,akimaanisha
ameshashiba.Rehema hakupinga kwani hata kabla ya kuongea hivyo alishamuhisi kwamba
tayari ameshashiba. Alimruhusu anawe mikono.Walimaliza kunywa chai na kupiga
story zao za kimasomo.
Bila
ya aibu ghafla Rehema alimtaka Mbaraka waingie chumbani ili wakaongelee mambo
yao humo kwa kumuhofia Janeth kujua kinachoendelea kati yao.
Mbaraka alianza kujawa hofu ila alikumbuka
maneno ya swahiba wake kwamba asisubutu kumuudhi Rehema kwani hiyo ni bahati ya
pekee.Alikubali na wakaingia chumbani.Mulikuwa na kitanda cha aina yake,alifikiria
aweze kufananisha na nini thamani ya chumba kile,aligundua thamani yake ni sawa
na ikulu ya viongozi wa nchi zilizoendelea.Rehema alimuangalia Mbaraka na
kugundua anahisi joto kiasi,alivuta pumzi ili kuondoa woga na
kumwambia aingie chooni aende kupunguza
joto kwa kujimwadia maji.Mbaraka alikaa
kama alikuwa anasubiria kauli hiyo
itoke kwani joto lilikuwa linamsumbua
sana licha upepo wa kiyoyozi kilichotumika chumbani humo.
Aliingia
chooni kama alivyokuja wala hakuvua chochote.Rehema alitaka kuitumia nafasi
hiyo ili aweze kuona maungo na mwili wote wa mwanaume huyo.Hisia za mapenzi
zilimzidi Rehema baada ya kuskia maji yakiwa yanamwagika chooni, alitumia akili
yake kujenga picha kwa kile kinachotendeka humo.Wakati wote huo alikuwa na
bashasha nafsini mwake ya kutaka kujua jawabu lake kutoka kwa ampendae.
Baada
ya akika kadhaa Mbaraka alitoka.Rehema alinyanyuka na kumsimamia mbele yake
mithili ya watu wanaotaka kupimana nguvu,ghafla bila kuhofia alisema “tafadhali Mbaraka unakumbuka ahadi yetu ya
usiku wa jana naomba unijibu ili niupe faraja moyo wangu…”,
Mbaraka aliuangalia uso wa Rehema kwa matao ya
chini kama aligundua amekosea kitu kisha alishika mikono yake na kumuuliza “hivi
Rehema kwanini unakuwa mgumu wa kuelewa na kumtambua mtu…?,nisingefanya
yote haya kama siko tayari kuwa nawewe
kwani ulishanieleza muda mrefu kama unanipenda…”.
Rehema hakuamini kama Mbaraka angesubutu
kumshika mikono yake na kumwambia maneno mazuri kama yale.Alitabasamu kisha
akamuuliza “unamaanisha nini?”.
Mbaraka
alijibu “namaanisha hatua yangu inakanyaga kila ukanyagapo mguu wako, nimekuja
hapa si kwa lengo jengine lolote ispokuwa nadhani Mungu ameshatuandika tufe pamoja…nakupenda sana Rehema”.
Rehema hakuweza kuamini anachokisikia,alihisi
kama kuna malaika aliyetumwa na Mungu aje amchukue na kumpeleka peponi.Ghafla
aliamua kumsogelea zaidi na kumkumbatia.Machozi yalimtoka kwa furaha na ule
uchungu wa kuteseka kwa muda mrefu ulipotea ghafla.Mbaraka alimtaka Rehema asiruhusu
chozi lake kudondoka kwani linamuumiza sana.
Kiukweli Rehema anampenda sana Mbaraka.Na sasa
Mbaraka ameshaukabidhisha moyo wake kwa mwenzake.Walikumbatiana kwa muda huku kila
mmoja akiwa na furaha ya kumpata yule ampendae.
Baada
ya dakika chache Rehema aliunyanyua uso wake kifuani kwa Mbaraka na kumuangalia
usoni ndipo alipoona machozi yakitiririka kutoka machoni mwa Mbaraka.Alienua mkono
wake na kuyapangusa.Furaha yao ilizidi kifani na kujikuta kila mmoja anaangua
kilio cha upendo wenye furaha.
Rehema
alimwambia Mbaraka “naomba nitimize ahadi nilioweka kwa Mungu”
Mbaraka
alishangaa na kujiuliza maswali bila kupata jawabu,“ahadi gani tena mpenzi
wangu” Mbaraka aliuliza kwa hisia.
“Niliweka ahadi kwa mungu kwamba endapo siku utakubali
ombi langu basi nakukabidhi nyumba yako binafsi, kwasababu tayari
nilishakuamini kwa kila kitu”.Mbaraka alifungua macho yake yote na
kushangaa,alihisi kama anaota akiwa amesimama mchana ule,“nyumba!!!” Aliuliza
kwa msangao.
Rehema alijibu “sio nyumba tu na hata uhai
wangu”.
Kwa
asilimia mia moja Mbaraka alizidi kuyasadiki maneno ya rafiki yake.Alimkumbatia
Rehema na kumwambia kwa sauti nyepesi pembezoni mwa sikio lake la kulia“Rehema
daima nautambua upendo wa dhati unapopatikana.Nimegundua upo kwako na ninakuahidi
kukutunza daima wala sitakuacha labda Mungu pekee achukue uhai wangu mapema
kabla yako”.
Rehema alizidi kufurahi na kuzidi
kuung’ang’ania mwili wa mpenzi kana kwamba hakutaka abanduke kifuani kwake.Walianza
kujikuta wanaanza kufanya vitu tofauti.Kila mmoja alianza kutembeza mikono yake
katika mwili wa mwenzake.Rehema alianza kurudi nyuma polepole na kujikuta wanaanguka
juu ya kitanda bila kujali.
Muda ulienda na ndipo Mbaraka alikumbuka
kwamba wakati huo alitakiwa awasili darasani.Ghafla alibanduka katika mikono ya
Rehema na kumwambia “Samahani ratiba inanibana muda huu si unamjua Yule mwalimu
Kesi anaweza kutoa kazi ya kushtukiza?”.Rehema hakufurahia kuambiwa vile kwani
tayari alishajiachia kwa kila ambacho kingetokea,ila kwa vile alikuwa anampenda
sana nakujali mafakio yake hakuwa na jinsi kumkubalia.Waliagana kwa mabusu
motomoto na kila mmoja kuwa na furaha na mwenzake.
Mapenzi
yao yalipamba moto na kujikuta wanaamua taarifa za uhusiano wao kuzipeleka kwa
wazazi wa Rehema kwaajili ya ndoa. Baada ya wazazi wa Rehema kuwasili nyumbani
walifurahia sana kupata taarifa hiyo ya mipango yao ya ndoa.Waliamini lilikua
ni jambo la kheri na Mungu angewazidishia baraka katika maisha yao.
Rehema hakuwa mnafiki kwa ahadi yake.Alimkabidhi
Mbaraka zawadi ya nyumba yenye thamani ya mamilioni ya fedha iliyopo maeneo ya
Mbezi.
Miaka ilisogea na penzi lao lilizidi kukuwa, hata
walifanikiwa kuhitimu shahada zao kutokana na bidiii zao.Mbaraka alifanikiwa
kupata ajira katika kampuni moja maarufu ya uuzaji na usambazaji wa magari
kutoka Japani akiwa kama msimamizi msaidizi wa kampuni hiyo maarufu iliyopo
Posta jijini Dar es salaam.
SURA YA NANE
Ilikuwa
jumapili majira ya saa tatu za asubuhi Mbaraka akiwa nyumbani kwake akijishughulishasha
na uandaaji wa chai,ghafla zilianza kumjia fikra juu ya wazazi wake,kwani tangu
aanze masomo yake ya chuo kikuu mpaka sasa ameshamaliza na kupata ajira
hajawahi kwenda nyumbani zaidi ya salamu kwa njia ya simu na kuwatumia fedha ili kukidhi mahitaji yao. Haikua
desturi mbaya kuwatumia pesa ila ni vyema zaidi aende nyumbani siku akipata
likizo kazini kuwaona wazazi wake waliofanikisha maendeleo na mafanikio yake.
Punde
simu yake iliita.Hakuwa mwengine bali ni baba mkwe wake mtarajiwa mzee Said
Lugomba.Aliipokea simu ile kwa heshima zote kwani alikuwa akimthamini na
kumuheshimu sana.
Mzee
nae alikuwa anampenda sana mkwe wake mtarajiwa.Alimtaka aweze kufika nyumbani
siku inayofuata asubuhi kwaajili ya kikao cha maandalizi ya ndoa.Hakulipinga
hilo zaidi ya kufurahi sana.Baada ya mawasiliano hayo alimpigia simu rehema na
kumjuulisha taarifa hizo punde tu kutoka kwa baba yake.Naye Rehema alifurahi
sana kusikia habari hiyo ambayo ilikua ndoto yake kwa muda mrefu.
Ama
kweli daima ngoja ngoja inaumiza matumbo.Kwa kipindi chote hicho kijiji cha Wasahawa
kilikosa furaha na amani.Kiliandamwa nahuzuni na vilio vya kuhuzunisha sana.Bahati
hakuwa duniani wala akhera, hakuwa anaelewa liendalo wala lirudilo duniani.Kwa
muda mrefu sasa yupo kitandani tu.
“Sisi tunampenda sana ila Mungu atampenda
zaidi”.Hayo ndio yalikuwa maneno ya waliowengi baada ya kuona kwamba Bahati hawezi
kupona.Alinyooka kitandandani mithili ya nyoka aliemwagiwa mafuta ya taa
kichwani pake.Alikuwa mwembamba aliyepoteza hata mvuto wa aina yoyote.Alikuwa
hatamaniki tena hata chembe, utadhani hakuwa mrembo na mlimbwende wa aina yake,alikwisha
kabisa,wazazi wake walishakata tamaa na kumsubiri Mungu amchukue siku
aliyopanga.
Kwa muda wote huo hawakujua ni nini haswa
kinamsumbua Bahati,hakuwa anaonekana na maradhi aina yoyote kila alipotazamiwa.Kifo
kilishaingia chumbani mwake,lakini moyo wake ulikuwa unafanya kazi moja tu yaupendo,kwani
bado Mbaraka alikuwa moyoni mwake.Hakuna alietambua hilo zaidi ya mzee Mkata pekee,nae
hakuweza kufichua siri hiyo ambayo alimuahidi kwamba atailinda na kuitunza
daima.Ugonjwa wa mapenzi ulizidi kummaliza Bahati kila muda ulivyokuwa unasonga
mbele.
Mzee Mkata alianza kujawa na huruma juu ya
maisha ya Bahati,alijuwa kwamba yeye alikua ndio mkombozi wa maisha yamwanawe,kwanini
na yeye asikomboe uhai wake.Aliwaza na kuwazua bila kupata jawabu lolote,ila
alitafakari kwa kina kwamba hata kama ataamua kumkomboa ataanzia
wapi.Alishindwa afanye niniila hakukata tama.
Siku ya jumatatu majira ya saa mbili asubuhi.Siku
ambayo ilitayarishwa kwalengo la kumtakia maombi Bahati.Wazee na na vijana walikusanyika
nje ya nyumba yao Bahati chini ya mti mrefu uliooteshwa kwa lengo la kuajiri
upepo na kivuli kizuri. Hakikuwa kikao cha furaha kwani kila mmoja alionekana
akiwa na huzuni zaidi ya mwenzake.
Mzee Mkata na mke wake nao hawakuwa nyuma, walionekana
wakikosa amani zaidi kwani wanampenda sana Bahati kwa tabia zake njema.Mkata
alionekana kukosa amani kabisa huku akiurai na kuushawishi moyo wake juu ya
hali ya ile. Baada ya dakika chache alisimama mzee mmoja aliyekuwa na kitambaa
mkononi mwake.Hakuwa mwengine bali ni baba wa mgonjwa huyo mahututi.Kitambaa hicho
hakikua kinatumika zaidi ya kufutia machozi.Aliwataka watu watulie na wae
tayari kumsikiliza.
“Sawa
mzee” watu waliitika kwa huzuni.
Alianza
kuwaambia “Bahati ndio yupo safarini kuelekea akhera, hivyo ninawaomba
wanakijiji nyote ambao mmumehudhuria hapa tutumie nafasi hii kumtakia dua kwani
hata mimi nimeshakata tama juu ya uhai wake”, alivuta pumzi kwa upole kisha
akaendelea “tuamini kwamba Mungu ndie mpangaji wa kila jambo,yeye ndie
anaemiliki pumzi zetu na kila kilichopo ulimwenguni,naamini sote tunaujua umuhimu
wa kuwepo binti yetu ila huenda Mungu amepanga tofauti na matakwa yetu.Naomba tumuombee
dua”. Mzee Hassan aliongea mengi zaidi ambayo yalizidi kuwapa watu masikitiko.Kila
mmoja alijiinamia chini kuficha sura yake iliyotokwa na machozi.Baadhi ya kina
mama walikosa nguvu na kujikuta wakilia kwa sauti kubwa huku wakipiga kelele
kana kwamba tayari Bahati ameshaiaga dunia.
Kijiji kilijiinamia kwa simanzi iliyotawala
kwa kila mmoja.Jambo hilo lilimfanya mzee Hassan kushindwa kuongea mengi.Aliamua
kukaa chini huku akijipangusa machozi kwa kutumia kitambaa chake ambacho
ameshika mkononi mwake.Ghafla mama wa Mbaraka alihisi kizunguzungu na kujikuta
akianguka katika bega la mume wake na kupoteza
fahamu.Tukio hilo lililozidi kumpa presha mzee huyo,alinyanyuka na
kushika kichwa cha mke wake huku akimlaza chini polepole akiwa hana fahamu
yoyote.Baada ya kuona tukio hilo mzee Hassan nae aliinuka mahala alipokuwa
amekaa na kumtaka mzee Mkata ashirikiane na kina mama wengine kumuingiza ndani.Nao
kwa haraka walifanya hivyo.Mzee Hassan alimuashiria mama Bahati asogee karibu
yake na kumtaka aende ndani ili akaandae sehemu ya kuweza kumuhifadhi jirani
yao kwa haraka.Aliingia ndani na kumtandikia eneo ambalo halikuwa mbali na Bahati
kisha alitoka nje kumuashiria mume wake kwamba tayari ameshafanya hivyo na
ndipo walishirikiana kumuingiza ndani.
Kweli usilolijua ni sawa na usiku wa giza kwani
baada ya mzee Mkata kuingia ndani aliangaza huku na huku katika purukushani
hiyo.Bila kutarajia alimuona Bahati akiwa amelala kitandani. Moyo wake ulizidi
kukatika kwa majeraha makubwa.Hakuweza kuvumilia tena maumivu ya kilasiku.Baada
ya kumlaza mke wake alimuomba mzee Hassan ampe japo dakika chache za kwenda
kumuona Bahati kitandani pale.Kwajinsi walivyokuwa marafiki hakuweza
kumkatalia.
Mzee
Mkata alisogea katika kitanda cha Bahati. Wakati alipokuwa akimtazama machozi
yalimtoka nakuhisi kwamba yeye ndio sababu ya Bahati kuwa katika hali hiyo.Alianza
kuyakumbuka yaleyote ambayo Bahati alimfanyia hadi kufanikisha ndoto za
mwanawe.Kutokana na upeo wa akili na busara zake alizokuwa nazo mzee huyo
aliweza kugundua kwamba mapenzi juu ya
Mbaraka ndio yaliyomsukuma Bahati kufanya aliyoyafanya hapo awali.
Aliwaza
mengi na kugundua kwamba maradhi ya Bahati yalianza punde tu pale Mbaraka
alipoondoka kwenda kusoma.Maswali yalikuwa mengi kichwani mwake na baada ya
kuunganisha matukio alipata jawabu kwamba maradhi ya Bahati ni kweli
yamesababishwa na Mbaraka kwani alimpenda ila inwezekana alishindwa kumweleza
na ndio mana yamemsibu maradhi yasio na tiba.
Maumivu
makali yalitoboa moyo wake, alijaribu
kumuamsha Bahati ili aweze kumuuliza japo alihisi kuwa asingemtambua kutokana
na kuugua maradhi hayo yaliyomkumba kwa muda mrefu.Alimuita kwa sauti ya chini
“Bahati...Bahati mwanangu ni mimi mzee Mkata nipo hapa…”. Kilichomshangaza ni
kumuona Bahati akilazimisha kufumbua macho yake na kuinua kichwa chake
akimtazama aliekuwa akiongea maneno hayo.Kwa bahati mzuri aliweza kuitambua
sura ya mzee huyo aliezoeana nae sana kipindi cha uzima wake.Alimzoea kwa
nidhamu yake ya kupita na kumsalimia kila siku aendapo shambani kuwasaidia
wazazi wake.
Mzee mkata alizidi kumtazama Bahati kwa huzuni
sana, wakati huo akiwa amesahau hali iliyomkuta mke wake na kwamba alihitaji
uwepo wake ili apone. Ghafla Bahati alitamka kwa sauti ya chini kumuuliza mzee
Mkata “umekuja na Mbaraka?”.
Mapigo
ya moyo ya mzee huyo yalipiga kwa kasi mithili ya ngoma iliyogongwa kwa nguvu
na kutoa mlio mkubwa uliosikika mbali.Aliamini kuwa alichokiwaza kilikuwa ni
cha kweli na hakuwa na sababu ya kusubiri na kuendelea kumuacha Bahati akizidi
kuteseka na kuichungulia akhera.Aliwaza vya kumjibu kwani alijua Mbaraka yupo
mbali na haijuilikani siku ambayo atakuja kijijini hapo.Aliamua kumdanganya ili kuupoza
moyo wake “Mbaraka yupo njiani anakuja kijijini kwajili yako,sawa mwanangu!!”,Bahati
alitabasamu.Kweli maradhi ya Bahati yalisababishwa na Mbaraka.
Mzee
mkata aliwaza kufanya mawasiliano na Mbaraka ili aweze kuja kijijini haraka
iwezekanavyo kuokoa maisha ya mtu aliyetimiza ndoto zake na mwenye upendo
wadhati kwake.
Alitoka
nje ya nyumba na kukuta wanankijiji wakiendelea kuulilia uhai wa Bahati.Kwa
busara alimuita mzee Hassan na kumtaka awaamuru wanankijiji kurejea majumbani
kwao.Ndipo wanakijiji walianza kutawanyika wakiwa wameshakata tamaa kuhusu
maisha ya mpendwa wao.
Wazee
hao waliitana pembeni kidogo ya nyumba na kuanza kuning’ona kwa sauti ya chini
sana,bila shaka kulikuwa na siri kubwa iliyokuwa ikijadiliwa na wawili hao.Kwa
mbali alionekana mzee Hassan akionesha sura ya mshangao wa jambo ambalo hakuwa mwenye kuliamini.Waliamua
kusogea pembeni zaidi na kukaa juu ya mkeka mkukuu ambao hata rangi yake haikuweza
kuonekana vizuri kwa jinsi ulivyokuwa umechakaa.Mzee Mkata alimueleza mzee
Hassan kwamba yeye anaelewa maradhi ya Bahati na alimtambua kwa muda mchache
ambao alimruhusu kuongea nae.Mzee Hassan alishangaa na kudhania kwamba Mkata
anaanza kuzeeka vibaya na labda akili zimeanza kumruka baada ya mke wake
kupoteza fahamu.Alimuuliza “unamaanisha nini mzee mwenzangu?,au meanza kula
chumvi nyingi sasa”.Mzee Mkata hakutaka kuongea mengi,alimtaka amsaidie
mawasiliano ili awasiliane na mwanawe Mbaraka kwa ajili ya kuja kijijini.
Kama
ilivyo kawaida ya Mzee Hassan, alikuwa anawajali sana wanakijiji kwa shida
alizoweza kuwasaidia,ghafla alinyanyuka na kuingia ndani,hakuchukua muda mrefu
alitoka akiwa ameshika simu ndogo mkononi mwake,alimkabidhi mzee Mkata na
kumtaka afanye anayotaka kufanya.
Wakati huo Mbaraka alishafika kwa kina Rehema
akisubiri kikao kianze kama alivyoahidiana na mzee Saidi.Kikao ambacho
alikwishaelewa dhamira yake ilikuwa ni matayarisho ya ndoa yake na mpenzi wake Rehema.Wakiwa
ukumbini yeye na mama mkwe wake pamoja na mke wake mtarajiwa wakimsubbiri mzee
Saidi afike ghafla simu yake iliita.Hakuwa mwengine ila ni baba yake kwani
alikuwa na kawaida ya kutumia simu ya Mzee Hassan pindi anapotaka kuwasiliana
nae. Kwa haraka na heshima aliipokea simu hiyo.Ila punde tu baada ya sekunde
chache uso wa Mbaraka ulionekana kuanza kupata huzuni kila alipokuwa anazidi
kuongea.Rehema alishtuka kumuona mpenzi wake amebadilika ghafla, alianza
kuelewa kwamba haikuwa simu ya furaha.
Mbaraka alikata simu na kubaki kama bumbuwazi.Rehema
aliwajibika kumtuliza na kutaka kujua nini kinaendelea.Nae mama mkwe wake
mtarajiwa hakuwa mbali na hilo alimshawishi Mbaraka aongee nini tatizo.Mbaraka
hakuona sababu ya kukaa kimya na kuzidi kupoteza muda bali aliwataka samahani
na kuwaambia kwamba alietoka kumpigia simu ni baba yake mzazi na anamtaka aende
nyumbani haraka iwezekanavyo.
Rehema alishtuka kusikia hivyo kwani alitambua
kwamba kutokana na ghafla hiyo hakutokuwa na salama.Mbaraka hakutaka kukaa sana
hapo ila aliamua kuenuka juu ya kochi,aliwaaga na kuwaambia wamvumilie na
wamsamehe kwa hili lililotokezea mpaka atakaporudi ndani ya siku mbili.
Kwa vile baba mkwe wake alikuwa hajafika hapo
aliwataka wampe salamu kwani Mbaraka alimuheshimu sana baba yake na hakuweza
kupinga chochote kutoka kwake katika hali yoyote ile.
Kutokana
kwamba hakujua nini kilichotokea huko aliamua kutekeleza na kuitikia wito huo
ipasavyo.
“Sawa
mwanangu safari nakutakia safari njema njema”.Maneno hayo yalisemwa na mamamkwe
wake mtarajiwa.
Wakati
anaondoka Rehema alimfata nyuma huku akiwa na huzuni juu ya wito wa Mbaraka kijijini.Alimtaka
waende wote lakini mbaraka hakupenda Rehema ajumuike katika safari hiyo
kwasababu hakujua anaitiwa jambo gani na alitegemea kurudi mapema tu kwasababu
yuko kazini.
Kwa vile Rehema alikuwa anatembea katika
kivuli cha Mbaraka ambae ni mume wake mtarajiwa hakuacha kuwa king’ang’anizi
juu ya hilo,hatimaye aliyaelewa maneno ya hekima ya mpenzi wake ambae alikuwa
ndoto yake kwa muda mrefu.Mbaraka alineua mikono yake na kumruhusu Rehema aweke
yakwake juu ya viganja vyake.Alishika mikono ya Mbaraka na kukumbatiana huku
mioyo yao ikiuma kwa kutaka kutengana kwa muda wa siku chache.Rehema alizidi
kutokwa na machozi mengi zaidi kwani hakujua ni nini ambacho kimejiri huko
kijijini. Lilikuwa ni fumbo lililoushinda moyo wake kulifumbua.
“sawa
safari njema mume wangu,elewa nakusubiri wewe tu kwa ajili yakufunga ndoa.”
mdomo wake ulijikaza kutamka hilo na kuiusia nafsi yake subra na uvumilivu juu
ya kiza cha siku chache.
“usijali
mke wangu,nitarudi kwa ajili yako baada ya siku mbili,siwezi kukuacha ukateseka
kwa ajili yangu,na hata mimi sitoweza kuutesa moyo wangu kwa kukaa mabli na
wewe.Nakupenda sana mke wangu,nisubirie”.Baada ya kuogea hayo Mbaraka alitoka
ndani ya nyumba hiyo ya kifahari na kuanza kutembea kwa mwendo wa unyonge
kuelekea barabara kuu kufikia kituo cha daladala.Wakati anatembea kichwa chake
kiliyageuza macho yake nyuma yakiwa yanamtazama Rehema aliekuwa nje ya geti akimsindikiza
kwa macho ya unyonge.
Mbaraka
alifika kituoni na kupanda daladala iliyokuwa inaelekea Mbezi.Alifika nyumbani
kwake majira ya saa sita za mchana.Aliingia chumbani kwake ili kujiandaa kwa
safari hiyo ya ghafla.
Baada
ya muda alitoka nje akiwa amevaa vizuri na begi dogo alilokuwa amelibeba
mgongoni kwake.Alitoa simu yake na kutuma ujumbe mfupi wa maandishi kwa bosi wake
wa kampuni ambayo anafanyia kazi ili kutaka kumjuilisha kuhusu safari hiyo ya
ghafla kwani alijua kwa wakati huo simu ya bosi wake haitakuwa hewani kutokana
na pirika za kikazi,hivyo asingeweza kuwasiliana nae.
Alisogea
kwenye kituo cha bodaboda,madereva wa bodaboda kama kawaida yao walichangamkia
kazi kama inzi wakati wakutapo chakula
chao wakipendacho.Mbaraka alichukuwa bodaboda kuelekea stendi ya mabasi Ubungo.
Aliwasili
stendi ya mkoa mnamo saa saba za mchana.Sauti za madalali wa mabasi ya abiria
ziliskika kwa wingi,kila mmoja alianza kumsogelea na kumpa sifa za gari lake
ili ashawishike nalo.Kelele zilikuwa nyingi ambazo ziliweza kusababisha hata
wengine kuanza kukingiana vifua kutokana na tamaa na njaa ya nchi yao.Mbaraka
alitoa simu yake na kuangalia muda.Kwakweli dakika na sekunde zilikuwa
zinatembea kwa kasi huku sauti za “Mbeya!!, Mbeya!!!, Iringa mapema, Moshi !!!,
Moshi!!!” zikisikika kwa fujo.Alisubiri asikiye sauti inayonadi Morogoro,nayo
haikuwa mbali kwani ilisikika ghafla “haya Morogoro!!Morogoro!!mapema”, aliifuata
sauti hiyo na kuanza kuchangamkiwa kama msanii maarufu kutoka ulaya.
Aliingia
ndani ya basi hilo huku mawazo mengi yakiwa yamemtawala kichwani mwake.Hakujuwa
ni nini haswa kimejiri nyumbani kwao.Wakati huo mawazo ya Rehema yalimjia
ghafla kutokana na mazoea na ucheshi wa mapenzi yao.
ANAEHITAJI KITABU HICHI TAFADHALI WASILIANA NAMI KUPITIA 0658745759.
BEI NI NAFUU SANA ELFU 5 TU.